Serikali Itaendelea Kushirikiana na Madhebu ya Dini Zote Nchini - Majaliwa
![]() | |||||||||||
Hivyo, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa dini zote na jamii kwa ujumla waendelee kuvumiliana na kustahamiliana hususan pale zinapotokea tofauti miongoni mwao, lengo likiwa ni kudumisha amani na ulivu uliopo nchini.
“Kuvumiliana na kustahamiliana ndiko kulikotufanya tuendelee kuwa wamoja na kuitunza neema hii kubwa ya amani katika nchi yetu. Kila mmoja wetu anapaswa kutambua kuwa anao mchango mkubwa katika kutunza na kuimarika kwa amani ya nchi yetu.”
Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo ya Mazazi ya Mtume Muhammad (S. A. W), Waziri Mkuu amesema kwamba hiyo ni fursa muhimu kwa waislamu wote kuyasoma na kuyatafsiri kwa kivitendo maisha ya Bwana Mtume katika mfumo wao wa maisha ya kila siku ili kuyafanya maisha yao hapa duniani yawe bora zaidi.
“Tukio hili la leo ambalo nimefahamishwa kuwa linafanyika kwa mwaka wa 25 sasa, ni kielelezo cha umoja, mapenzi na undugu miongoni mwetu. Katika Quran Surah ya 49 (Al-Hujurat) ayah ya 10, Mwenyezi Mungu anatufahamisha kuwa ’hakika waumini ni ndugu.......’ Kwa msingi huo, tukiwa Waislamu suala la kuimarisha umoja, undugu na ushirikiano katika nyanja zote ni wajibu wa kila mmoja wetu.“
Kadhalika, Waziri Mkuu ameongeza kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) naye katika kusisitiza suala hilo la umoja, kwenye hotuba yake ya kuaga alihimiza kuwa mtu yeyote yule hawezi kuwa bora dhidi ya mwingine kwa sababu tu ya rangi yake au kabila lake lakini kitu pekee kitakachompa yeye daraja hilo la kuwa bora ni kutenda haki na kumuogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Awali, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakari Bin Zuberi alisema katika kuadhimisha Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) waislamu nchini wanapaswa waendelee kuwa watulivu na wasikivu wa kila jambo linalotolewa kwao na viongozi.
Maadhimisho hayo yamehudhuliwa na masheikh na viongozi wa Serikali kutoka maeneo mbalimbali nchini. Pia yamehudhuriwa na masheikh kutoka nchi za Paksani, Iraq na Misri ambao kwa ujumla wao wameisifu Serikali ya Tanzania kwa kudumisha amani, umoja, utulivu na mshikamamo.




