Breaking News

Chadema Kanda ya Pwani Yaitaka Serikali kuongeza Umakini Mapambano Dhidi ya CORONA


CHAMA cha maendeleo na Demokrasia CHADEMA kanda ya Pwani kimebaini changamoto za vitakasa mikono kwenye vituo vya magari ya mwendokasi katika kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Corona na kuiomba serikali kufanya uchunguzi pamoja na kuwachukulia hatua.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana msemaji wa kanda ya pwani Gerva Lyende alisema pamoja na jitihada ambazo zimekuwa zikichukuliwa na serikali kukabiliana maambukizi ya ugonjwa wa Corona chama hicho nimepata taarifa kuwa baadhi ya vituo vimekuwa vikitumia maji ya jiki kunawia mikono badala ya sanitizer.

"Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha inazuia na kutokomeza kabisa ugonjwa huu nchini ila kumekuwepo na baadhi ya watumishi ambao sio waaminifu wamekuwa wakihujumu jitihada hizo," alisema Lyende

Lyende alisema kuwa serikali inatakiwa kuongeza umakini na kuchukua tahadhali kubwa sambamba na kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kwa lengo la kuhakikisha maambukizi hayo yanapungua ama kumalizika kabisa nchini.

"Napenda kutoa ushauri kwa serikali kuongeza umakini zaidi katika suala hili sambamba na kushirikisha sekta binafsi dhidi ya mapambano ya ugonjwa  huo  na kuangalia namna ya upatikanaji bidhaa  kama sanitariza kwa bei nafuu katika kipindi hiki.

Aidha msemaji huyo amewataka viongozi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kanuni za uongozi badala ya kuzikiuka kwani kufanya hivyo kutaisaidia jamii kuendelea kuwa na umoja katika mambo mbalimbali ambayo yatasaidia kuleta amani umoja na mshikamano.

Alieleza kuwa baadhi ya nchi kama Uganda wameweka sheria ambazo zimewataka watu kuzifuata hususani kwenye mikusanyoko ya watu kama katika vyombo vya usafiri na masokoni na wanaokiuka ama kukaidi huchukuliwa hatua kali.

Kiongozi huyo amewasahi baadhi ya viongozi kutofanyia mzaha suala hilo la Corona kwa kuwa limekuwa likiteketeza maelfu ya watu na kuacha familia nyingi zikiwa kwenye majonzi kwa kuondokewa na wapendwa wao.

Ametoa wito Kwa serikali kuhakikisha inatoa vitakasa mikono santaiza kwa wananchi ama kuongea na wauzaji kwa lengo la  kupunguza bei ya bidhaa hiyo ambapo kwa sasa huuzwa chupa ya mililita 250 kwa kiasi cha shilingi elfu 10.