Waziri Jenista Mhagama Akabidhi magari 12 kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2020
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama kwa niaba ya Serikali amekabidhi magari 12 kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani wa Tanzania Bara. Magari hayo ni sehemu ya magari 20 ambayo yamenunuliwa na Tume.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi magari hayo, Mhe. Mhagama amesema Serikali itahakikisha kwamba Tume inawezeshwa kufanya kazi zake kwa mujibu wa Katiba na Sheria ili iweze kuendesha uchaguzi ulio huru na wa haki.
“Kwetu sisi kama Serikali wajibu wetu wa kwanza ni kuhakikisha kwamba Tume haikwami katika kutekeleza majukumu yake, hata fedha zinazohitajika katika shughuli zote za uchaguzi zinatengwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali,” amesema Mhe. Mhagama.
Aliipongeza Tume kwa weledi katika utendaji kazi na kusema kwamba msingi wa uhuru wa Tume uliowekwa na Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 utaendelea kuheshimiwa na Serikali.
“Nchi kama Malawi na nchi nyingine zinakuja kujifunza kwenye Tume hii, nakupongeza sana Mwenyekiti (wa Tume) na wafanyakazi wote. Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ametamka kwamba mwaka huu tuna uchaguzi na ametamka kwamba uchaguzi huo lazima uwe huru na haki. Magari haya 12 mmepata, mtapata magari mengine nane (8) na sio magari tu bali vifaa vyote vya uchaguzi vimeshafikia hatua nzuri ya manunuzi, fedha zimeshatengwa,” alisema Mhe. Waziri
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (mst) Semistocles Kaijage ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa Tume ili iweze kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba na Kisheria.








