Breaking News

NEC Yatangaza Tarehe Awamu ya Pili ya Kuboresha Daftari la Wapiga Kura 17 April hadi 4 Mei 2020


Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekutana na wawakilishi wa Vyama vya Siasa Jijini Dar es Salaam na kutangaza rasmi tarehe ya kuanza kwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili ikiwa ni pamoja na uwekaji wazi wa Daftari la Awali. 

Mwenyekiti wa Tume, Jaji Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage amesema mazoezi hayo mawili yatafanyika sambamba kuanzia tarehe 17 Aprili 2020 na kukamilika tarehe   4 Mei 2020.
Alisema mazoezi hayo yatafanyika kwa routes (awamu) mbili na route ya kwanza itajumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mara, Simiyu , Mwanza, Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma na Tabora  kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili 2020. 

Route ya pili itajumuisha Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara kwenye mikoa ya Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Iringa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam kuanzia tarehe 02 hadi 04 Mei 2020
Kwenye mkutano huo vyama vya siasa vimekabidhiwa orodha ya vituo vitakavyotumika katika zoezi hilo la uboreshaji wa Daftari.

Aidha, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Dkt. Wilson Mahera Charles amesema kutokana na uwepo wa ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona Tume imechukua tahadhari zote muhimu za kiafya ili kuhakikisha usalama wa wananchi watakaojitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao.