Breaking News

RC Makonda: Wazururaji Watakaokamatwa Kupewa Adhabu ya Kusafisha Mazingira na Kazi za Kijamii


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda ametoa ufafanuzi juu ya zoezi la kuwakamata wazururaji ambalo limeanza rasmi leo ambapo wazururaji watakaokamatwa watapewa adhabu mbalimbali ikiwemo Kusafisha mitaro, Kusafisha barabara, kufyeka nyasi na kulima bustani.

Akizungumza mara baada ya Uzinduzi wa Shoppers Supermarket ya Mlimani City jijini Dar es salaam alisema kumekuwepo na baadhi ya watu kutokuelewa kauli yake hiyo na kueleza kuwa kama kuna watu walidhani watapelekwa mahabusu na kula Chakula cha bure wasahau kabisa jambo hilo.
Mara baada ya kutoa kauli kuanza zoezi la kuwakamata wazururaji kumeibuka watu ambao wamekua wakitoa mitizamo yao na wengine kupotosha hasa katika mitandao ya kijamii ila ieleweke kuwa wale wote watakaokamatwa watatafutiwa kazi za kufanya maeneo mbalimbali ya kijamii" Alisema mhe. Makonda.

Pia mhe Makonda amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao kwa kuzingatia na kufata ushauri uliotolewa na wataalam wa afya katika kipindi hiki cha maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona-19 badala ya kukaa ndani kwa kutafuta sababu zisizo na tija.
Katika hatua nyingine  mhe. Makonda ameonyesha kuridhishwa na kufurahishwa na uwekezaji uliofanyika na wazawa jambo lililosaidia zaidi ya Vijana 205 kupata Ajira kwa Shoppers ya Mliman City pekee.

Alisema uwepo wa Supermarket hiyo licha ya kuwezesha wananchi kupata mahitaji muhimu pia serikali inapata Kodi ambapo inaelezwa kwa kipindi cha miezi nane pekee ambayo Jengo hilo kikifungwa serikali ilikosa kodi ya shilingi Bilioni 28.

Aidha  mhe Makonda aliongeza kuwa kuwepo wa Supermarket hiyo pia utawezesha Wafugaji na Wakulima wa Mazao ya Matunda na Mbogamboga kupata sehemu ya kuuza Mazao yao.