Breaking News

TAMWA: Tunaamini Uchaguzi Mkuu Utakuwa Huru na Haki

 Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na WILDAF pamoja na Global Peace Foundation GPF wameridhishwa na hatua na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa viongozi kuhimiza uchaguzi huru wa haki na usawa pamoja na kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea wote.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es salaam kuhusu changamoto zilizoibuliwa katika mdahalo wa wagombea wanawake na wanasiasa wa siku mbili, mkurugenzi mtendaji wa TAMWA Rose Reuben, alisema kati ya wagombea 16 waliochukua fomu za kugombea nafasi ya Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kati yao wanawake ni wawili.

Alisema katika mdaharo washiriki walijadiliana na kutoa mapendekezo kwa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi kuondoa changamoto zote zinazochagiza ushiriki duni wa wanawake katika siasa.

"Katika mdahalo huo wa siku mbili ambao uliwakutanisha wanawake wanasiasa ulijadili changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo ambazo zimekuwa kikwazo kwao jambo linalopelekea kuwepo na ushiriki duni wa wanawake kujitokeza kugombea" Alisema bi Rubeni.

Alisema katika utafiti uliofanya na chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA), WILDAF na GPF chini ya ufadhili wa mfuko wa Maendeleo Wa Wanawake Afrika (AWDF) kupitia mradi wa WANAWAKE SASA wamebaini bado kuna changamoto zinazopelekea ushiriki mdogo wa wanawake katika siasa, baada ya kuendesha midahalo mbalimbali.

Wanawake wanaogombea nafasi za uongozi, hukutana na changamoto nyingi zikiwemo lugha kudhalilisha wakati wa kampeni na hata wakati utendaji wao wa kazi ili kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma

“Kama tunataka uchaguzi huru na haki, na wa kidemokrasia ni muhimu kwa tume ya uchaguzi na vyombo vya usalama kupiga marufuku na kutoa adhabu kali kwa wanasiasa watakaotoa lugha za udhalilishaji dhidi ya wanawake” . Amesema Rose.

Katika hatua nyingine mkurugenzi mtendaji wa TAMWA, ametoa rai kwa wanawake kukataa kudhalilishwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ya fedha au ngono.