LHRC Na TCAFGM Waishauri Serikali Kufuta Sheria Kandamizi Za Kimila Zinazokandamiza Wanawake Vijijini

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Mtandao wa Kupinga Ukeketaji Tanzania (TCAFGM) kimeishauri serikali kufuta sheria za kimila zinazo mkandamiza mwanamke hususani wa kijijini.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wanawake vijijini yalioandaliwa na kituo hicho kwa kushirikiana na mtandao huo kwa kuhamasisha wadau wa vijijini, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Bi. Anna Henga, alisema katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake wa vijijini, ni vyema jamii ihakikishe inaachana na mila potofu na zilizopitwa na wakati ili kuhakikisha haki za wanawake wa vijijini zinalindwa ipasavyo.
Alisema kutokuwepo na usawa wa kijinsia kunachangia kutaharakisha maendeleo hususani vijijini ambapo kuna idadi kubwa ya wanawake, kwani Tanzania asilimia 77.9 ni wanawake wa vijijini na 22.1 ni wanawake wa mijini.
"Serikali inapaswa kuunda vikundi mbalimbali vya wanawake vijijini na kuwajengea uwezo kuhusu haki zao na pia kuwapatia fursa mbalimbali za kimaendeleo" Alisema Bi Henga

Nae Mwenyeketi wa Mtandao wa Kupinga Ukeketaji Tanzania, Bi Sarah Mwaga alisema kuwa licha ya Tanzania kuchukua juhudi za makusudi kuhakikisha wanafikia usawa wa kijinsia lakini bado wanawake wa vijijini wamekua wakipitia changamoto nyingi ambazo bado zinahitaji juhudi zaidi za kuweza kuwasaidia.
Wanawake wa vijijini wamekua wakipitia changamoto nyingi ikiwemo sheria kandamizi hasa katika masuala ya mirathi na ndoa, Umiliki wa ardhi vijijini pamoja na kuwepo desturi zilizopitwa na wakati.
“Kuwepo kwa mfumo dume ambao umeshamiri hususani vijiji, ukosekanaji wa huduma bora za afya, elimu, kutoshiriki wanawake wengi hasa katika ngazi za maamuzi na uongozi,kuwepo kwa ajira za utotoni pamoja na wengi kukosa haki zao kutokana na elimu kuhusu haki zao hizi ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanawake wa vijijini”alisema Bi. Sarah



