12 MBARONI KWA WIZI WA NJIA YA MTANDAO NA UTAPELI
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 12 kwa kujihusisha na utapeli na makosa ya wizi kwa njia ya mtandao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Muliro Jumanne Muliro amesema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya Jeshi kwa kushirikiana na polisi wa mikoa na Mamlaka zingine za Serikali kufanya Operesheni maalum kuanzia Februari 6 hadi Februari 20 mwaka huu.
Amemtaja mmoja wa watuhumiwa kuwa ni Rajabu Hamisi, miaka 34, Mnyaturu, mkazi wa Rau Moshi Kilimanjaro na wenzake 11 ambao wamekuwa wakijihusisha na wizi huo.
“Watuhumiwa hao walikutwa na Laptop moja mali ya Kampuni ya Tigo, EFD mashine moja, Simu za mkononi 42, kadi za Tigo (line) 55, nyaraka zenye kurasa 1500 ambazo ni taarifa za mawakala wa mtandao wa Tigo nchi nzima, nyaraka zenye taarifa za wateja wa CRDB,” amesema ACP Muliro.
Kamanda Muliro amebainisha kuwa vielelezo vyote hivyo walikuwa wakivitumia kufanyia wizi kupitia kwa mawakala na mteja mmoja mmoja kwa kuwapigia simu au kuwatumia ujumbe wakijifanya ni wafanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi na kisha kutoa maelekezo ambayo hupelekea mteja au wakala kuwatumia pesa wahalifu hao.
Amafafanua kwamba wakati mwingine wezi hao hutoa maelekezo kwa kujifanya wanahuisha mfumo wa kampuni wanaokutajia na mwisho hukuelekeza kuweka namba yako ya siri baada ya hapo mhusika hujikuta ameibiwa pesa kutoka kwenye akaunti yake.
Hivyo Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi kanda Maalum ya Dar es salaam linawataka watu wote walioibiwa kwa njia ya mfumo huo wafike Kituo cha Polisi Oysterbay ambako upelelezi wa watu hao unaendelea ili taratibu za kisheria zikamilishwe na wafikishwe Mahakamani.
Wakati huo huo ACP Muliro amebainisha kuwa Jeshi hilo linamshikilia pia Haji Mussa, umri 30, Muha, mkazi wa Chamazi Temeke kwa tuhuma za kumshambulia kwa fimbo na kumsababishia maumivu makali mtoto wake wa kambo aitwaye Feisali Deogratias Masawe, miaka 11, Mchaga, Mwanafunzi wa Darasa la tatu Shule ya Msingi Chamazi Dovya.
“Alimtuhumu kuwa amemuibia shilingi 195,000, usiku wa tarehe 22.02.2022. Tarehe 23/02/2022 Mtoto Feisali Deogratias Masawe alifika Shuleni na ilipofika majira ya saa sita na nusu alidondoka na kupoteza fahamu. Alipelekwa hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo anaendelea kupatiwa matibabu,” amesema ACP Muliro.
Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha Mtoto huyo kuumwa ni kipigo alichokipata kutoka kwa baba yake wa kambo.
Amesema kitendo alichofanya mtuhumiwa ni cha ukatili uliopita kiasi na Jeshi haliwezi kuvumilia vitendi hivyo na kwa sababu hiyo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.
Vile vile ameeleza kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linamshikilia mtuhumiwa mwingine wa jinsia ya KE (jina limehifadhiwa kwa upelelezi) kwa tuhuma za kukutwa na Magari mawili ya wizi aina ya Toyota Land Cruiser Hard Top pamoja na T. 588 DJR Toyota Land Cruiser LX mali ya Dkt. Danstan Sebastian Kabelwa lililoibwa kati ya Januari 7 na Februari 13 mwaka huu maeneo ya Yombo Vituka Temeke.
“Upelelezi unakamilishwa ili Wahusika wote waweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema.
Katika huo huo Kamanda Muliro amesema Jeshi pia lilikuwa linafuatilia kwa karibu tukio la wizi lililotokea tarehe 13/02/2022 majira saa nane usiku katika Hoteli ya Keys Ilala ambako Mukupa Nabaloli, jinsia Ke, miaka 40, Raia wa Congo akiwa amelala katika Hoteli hiyo aliibiwa kiasi cha Dola za Marekani (USD) 3000/=, Laptop nne mpya aina ya Lenovo zenye thamani ya Dola za Kimarekani 1000/= na pesa za Kitanzania Tshs 230,000/=



