Breaking News

LHRC YAIPONGEZA SERIKALI KUFUNGUA MILANGO YA MAJADILIANO NA WADAU WA HABARI

Kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC kimeipongeza kauli ya Serikali kupitia waziri wa habari, Mawasiliano  na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye ya kufungua mlango wa majadiliano kati ya wizara na wadau wa habari kwa lengo la kufanya maboresho ya sheria za habari pamoja na kuyafungulia magazeti yaliyokuwa yamefungwa.

Akizungumza jijini Dar es salaam, mkurugenzi LHRC, wakili Anna Henga  alisema hatua hiyo ya serikali inaonyesha uwepo wa dhamila ya dhati katika utekezaji wa kauli ya mhe rais Samia Suluhu Hassan April 6 2021 wakati akiwaapisha makatibu na manaibu wakuu na wakuu wa taasisi za serikali na  alipokutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari june 28 2021.

"Kauli ya mhe Waziri Nape Nnauye alitoa tamko hilo wakati wa Semina na Wahariri iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)," Alisema Wakili Henga

Alisema LHRC ikiwa mdau wa sheria za habari imefanya uchechemuzi kwa muda mrefu tangu kuibuka kwa wimbi la utungaji wa sheria zinazoweka ugumu kwa vyombo vya habari kufanya kazi zake.

"Pia kwa kiwango kikubwa Sheria hizo zimekwamisha urahisi wa upatikanaji wa taarifa kwa jamii. Miongoni mwa sheria hizo ni Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015, Sheria ya Upatikanaji wa Habari, 2016, Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano pamoja na kanuni zake, na Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari, 2016,".

Wakili Hanga aliongeza kuwa bado Sheria hizo zimekuwa zikieendelea kuathiri utendaji wa vyombo vya habari, hivyo tamko la Waziri Nape ni kiashiria kizuri cha kurudi kwa uhuru wa vyombo vya habari na ni muda muafaka sasa kuangalia changamoto za kiujumla za sheria zinazoikabili Sekta ya habari na uhuru wa kujieleza.

"Ukiangalia kurejeshwa kwa leseni za magazeti manne gazeti la MwanaHalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima kufuatia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan. Lakini kulikuwa na maagizo ya Mahakama kufunguliwa kwa magazeti yaliyofunguliwa,"

Aidha LHRC imetoa wito kwa Serikali kuunda kikosi kazi kupitia upya na kutekeleza maamuzi ya Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya 2016.