Breaking News

MAJALIWA: TARURA SIMAMIENI MIRADI KWA WELEDI NA UAMINIFU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wahandisi wa TARURA wasimamie miradi kwa weledi, uadilifu na uaminifu huku wakizingatia mikataba husika na pia wawe wabunifu kutumia teknolojia mpya, sahihi na rafiki kulingana na upatikanaji wa malighafi za ujenzi.
 
“Pia ninaisisitiza TARURA kufanyia kazi haraka, maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kujifunza teknolojia inayotumiwa kutengeneza barabara za Zanzibar ambayo imeonesha kuwa nafuu na ya viwango vya juu.”  
 
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Februari 12, 2022) alipofungua Mkutano wa Kazi kati ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI, TARURA, Wakandarasi, Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, Mfuko wa Barabara na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma katika Ukumbi wa Mtakatifu Gasper, Dodoma.
 
Amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuijengea uwezo TARURA ili iweze kutekeleza makujumu yake ikiwa ni pamoja kuiongezea fedha kutoka sh. bilioni 247.5 ilipoanzishwa mwaka 2017 hadi kufikia Sh. bilioni 752.61 sawa na ongezeko la asilimia 204.3.
 
“Fedha hizo zinajumuisha sh. bilioni 127.50 kutoka Serikali Kuu, sh. bilioni 272.50 kutoka Mfuko wa Barabara, sh. bilioni 322.15 kutoka katika tozo ya sh. 100 kwa lita ya mafuta ya petroli na dizeli na sh. bilioni 30.44 kutoka kwenye ushuru wa maegesho wa magari.”
 
Amesema mwaka 2017, TARURA ilikuwa inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 108,946.19 na sasa mtandao huo umeongezeka na kufikia kilomita 144,429.77 ambazo zimetangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali Na. 463 la tarehe 25 Juni 2021.
Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa wakati TARURA inaanzishwa mwaka 2017, barabara za lami zilikuwa kilomita 1,449.55 sawa na asilimia 1.30 na sasa ni kilomita 2,473.55 sawa na ongezeko la kilomita 1,024 sawa na asilimia 70.6.
 
Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ifuatilie na kuchukua hatua stahiki kwa Halmashauri zote zitakazoshindwa kutekeleza kazi za matengenezo ya barabara kulingana na mkataba wa makubaliano (Annual Performance Agreement).
 
Mheshimiwa Majaliwa ameagiza usanifu wa miradi yote ya vipaumbele ufanyike mapema badala ya kusubiri mpaka fedha zipatikane na hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa watendaji wote wanaothibitika kusababisha kazi mbovu na upotevu wa fedha za TARURA.

“Usimamizi wa taratibu za utoaji wa zabuni ufanyike kwa umakini na kwa kuzingatia sheria. Mikataba ya kazi isainiwe kwa wakati, pia tathmini za zabuni zizingatie Sheria ya Ununuzi wa Umma na zihusishe upekuzi ili kupata makandarasi wenye uwezo na kukidhi vigezo stahiki".

Pia, Waziri Mkuu amesema TARURA ianze kutekeleza mpango wa uwekaji taa za barabarani wakati wa ujenzi wa barabara. “Hakikisheni hii inakuwa sehemu ya mkataba wa ujenzi wa barabara zote zinazojengwa, jifunzeni utaratibu huu kutoka TANROADS ambao tayari wanautekeleza”.

Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wazawa wajiimarishe katika kazi zao za ujenzi wa barabara ili waweze kufanya kazi yenye ubora, kwa wakati na viwango. “Wakandarasi mnaoomba kazi ni vyema mkajiridhisha na aina, ukubwa, mazingira ya eneo la kazi na kazi mnazoomba ili muweze kujaza gharama za mradi kulingana na uhalisia.