WAZIRI GWAJIMA AIPONGEZA BRAC MAENDELEO TANZANIA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima leo ametembelea miradi ya watoto inayotekelezwa na Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania.
Akizungumza baada ya kutembelea vituo hivyo Waziri Gwajima amelipongeza Shirika hilo kwa kazi nzuri iliyayofanya ya kujenga vituo vya makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto.
“Niwapongeze kwa mradi huu na mmeahidi hadi Juni vituo vyote vitakuwa vimekamilika. Vituo hivi ni muhimu kwa usalama wa kiakili na kimwili kwa watoto wetu,” amesema Dkt. Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima ameahidi kuwa Serikali itashirikiana na Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania ili kuhakikisha mradi unakamilika hivyo ameomba wakae pamoja na kujadili kabla ya bajeti ili kuona ni namna gani Serikali itawezesha mradi kukamilika.
Amesema vituo vyote vya ECD katika mradi huu vimejengwa kwa ufadhili wa Shirika la Tuzo ya Yidan la Korea na kutumia mtaala wa michezo ambao uliundwa na BRAC kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) na wadau wengine wa watoto.
“Mtaala huu unaotumia michezo kufundishia unatumia mfano wa mradi wa Play Lab uliotengenezwa na BRAC na kutekelezwa katika mikoa ya Mbeya, Tanga na Dar es Salaam. Mtaala huu ulichaguliwa kwa sababu ya njia yake ya ubunifu ya kuhakikisha fursa bora za kujifunza kwa gharama nafuu kwa watoto hasa walio katika mazingira magumu. Mradi huu hutumia michezo ya ndani na nje ya darasa ili kuwapa watoto ujuzi na na pia kuwaandaa kwa shule za msingi,” Alisema Bi. Bipa.
Kwamba baada ya kuhitimu kutoka vituo hivi, watoto wataingizwa kwenye madarasa ya awali katika shule za serikali husika ambapo BRAC itaendelea kutoa msaada wa kiufundi ili kujenga uwezo wa walimu wa awali.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa tangu mwaka 2016 BRAC ilipoanzisha mfumo wa kufundisha kupitia michezo kupitia mradi wa Play Lab, zaidi ya watoto 3,500 wenye umri wa miaka mitatu hadi mitano kutoka BRAC Play Labs katika mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya wameingizwa katika shule za msingi.
“Pamoja na mradi wa EELAY unaotekelezwa katika mkoa wa Tanga ECD, zaidi ya watoto 1670 wamejiunga katika shule za msingi 35 katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Tanga,” ameeleza Bipa.
Waziri Gwajima pia alitembelea mradi mwingine ambao ni Mpango wa Taifa wa Msaada kwa Mtoto–National Child Help Line ambao unatekelezwa na Shirika la C-Sema kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ambao unawasaidia watoto wanaohitaji huduma na ulinzi kupitia laini ya simu isiyo na malipo ya 116 inayopatikana katika mitandao yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwaka 2020, BRAC Maendeleo iliungana na C-Sema kuunga mkono mpango huu kupitia ufadhili kutoka kwa LEGO Foundation, ikiwa ni kama muendelezo wa mpango wa BRAC katika kusaidia maendeleo ya watoto wadogo nchini.
Kituo cha simu cha C-Sema kinasaidia utunzaji wa watoto wenye umri wa miaka 0-8 na wazazi wa watoto wote, kuwapa kipaumbele wale walio katika hatari na kutengwa sana. Kituo pia kinajulisha jamii na walezi kuhakikisha afya na lishe bora ya watoto, na kuwalinda kutokana na vitisho na hatari. Zaidi ya hayo, kituo kinawapa watoto wadogo fursa za kujifunza, kupitia mwingiliano ambao ni msikivu na wa kihisia na pia kusaidia afya ya akili na ustawi wa walezi.
Picha mbalimbali za matukio ya ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea miradi ya watoto inayotekelezwa na Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania leo Machi 2, 2022 mkoani Dar es Salaam



