WAZIRI MBARAWA AAGIZA TRC KUKAMILISHA UJENZI WA JENGO LA STESHENI KUU YA DAR
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameagiza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha jengo la stesheni ya kuu ya Dar es Salaam katika mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) linakamilika.
Profesa Mbarawa ameabainisha hayo leo Machi 3, 2022 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa SGR.
“Tumeona ni jengo zuri na litakamilika hivi karibuni lakini maelekezo yangu ya kwanza hili jengo limalizike mara moja. Tumekuwa tukisema kila siku linamalizika hivi karibuni, hivi karibuni, karibuni haifiki? Amehoji Waziri Profesa Mbarawa.
“Sasa muda umefika kama tunasema mwezi wa nne, mwezi wa nne liwe limekamilika, hatuwezi tukaenda kila siku kesho kesho Watanzania hawatatuelewa,” ameongeza.
Alisisitiza kuwa jengo hilo ni zuri sana ambalo limejengwa kwa vifaa vizuri na miundombinu mizuri, hivyo ni lazima wawe na utamaduni wa kulisimamia ili liendelee kuwa imara katika ubora wake.
“TRC walisimamie jengo hili vizuri, Msanja umeniambia kutakuwa na mtu maalum ambaye atakuwa analisimamia hili ni jambo jema. Lakini ili kulisimamia vizuri ni lazima kuhakikisha usafi unafanyika kama unavyotakiwa, kama ni mifumo iende kama inavyotakiwa. Mfumo unaweza kuharibika lakini haraka iwezekenavyo uweze kutengenezwa,” amesema Prof. Mbarawa.
Aidha amesema kuwa kuwe na utaratibu wa kulifanyia ukarabati jengo hilo ili liendelee kuwa imara.
Mwonekano wa jengo la Stesheni Kuu ya Dar es Salaam



