Breaking News

CUF YAWASILISHA MAPENDEKEZO KIKOSI KAZI CHA RAIS SAMIA

Chama cha Wananchi (CUF), kimependekeza mchakato wa upatikanaji katiba mpya ufufuliwe mara moja na kushauri kamati maalumu ya watalaamu iundwe kwa ajili ya kutekeleza shughuli hiyo.

Ujumbe wa CUF ulioongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Prof. Ibrahim Lipumba, kimewasilisha mapendekezo  hayo katika Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan, leo Jumanne, jijini Dar es Salaam.

“Inawezekana kuunda tume au kamati maalum itakayojumuisha wawakilishi kutoka vyama vya siasa, madhehebu ya dini, Asasi za Kiraia na kupata tume yenye muafaka wa kitaifa. Tume hii itaweka mezani  Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba na Katiba inayopendekezwa na kupata Rasimu ya Katiba ya Maridhiano, itakayopitishwa na Bunge na hatimaye kupigiwa kura za Maoni na wananchi,” imesema taarifa ya CUF.

Mbali na uundwaji wa tume hiyo, CUF kimeshauri Sheria ya Kura ya Maoni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, zifanyiwe marekebisho, ili ziendane na wakati.

Pia, kimeshauri muundo wa Serikali na mjadala wa rasimu ya katiba, upewe kipaumbele kufanyiwa kazi katika chakato huo.

Katika hatua nyingine, CUF kimependekeza katiba iliyopo ifanyiwe marekebisho madogo, kwa ajili ya uundwaji tume huru ya uchaguzi kabla ya chaguzi zijazo.

Kuhusu mikutano ya hadhara, chama hicho cha upinzani kimeshauri Jeshi la Polisi liondolewe katika usimamizi wa suala hilo, badala yake lisimamiwe na Sheria ya Vyama vya Siasa. 

Pia, Kimeshauri viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais, wasipewe mamlaka ya kuzuia mikutano ya hadhara.

Hali kadhalika, hama hicho kimependekeza masuala mbalimbali kuhusu chaguzi, kikitaka suala la wadhamini kwa wagombea, uhalali wa mawakala wa uchaguzi, yaondolewe kwenye matakwa ya kisheria,  badala yake yaamuliwe na vyama vya siasa.

CUF kimependekeza mapingamizi na rufaa katika chaguzi, yasikilizwe na kutolewa uamuzi ndani ya siku 14, huku kikishauri suala la mgombea kupita bila kupingwa liondolewe badala yake kuwe na kura ya ndiyo au hapana.