TCRA YATOA UFAFANUZI JUU YA BEI ZA HUDUMA ZA MAWASILIANO
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa ufafanuzi kufatia kuwepo na malalamiko katika mitandao ya kijamii juu ya mabadiliko ya bei hasa za huduma za data nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari alianza kutoa ufafanuzi kuwa bei za huduma za mawasiliano ya simu nchini zimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni bei za kawaida na bei za huduma ndani ya vifurushi.
Alisema huduma za vifurushi zinaambatana na masharti ya kikomo cha muda pamoja na matumizi ambayo ametolea mfano kuwa ni vifurushi vya siku, wiki, mwezi, vya wanachuo, vya siku, vya maneno maalum na kadhalika ambavyo huwa vinabadilika kutokana na uhitaji.
“Vifurushi ni sawa na “buffet”, ambapo mteja anaweza kula au kunywa chochote kilichopo kwenye “package” hiyo ndani ya muda maalum,” Alisema Dkt. Bakari.
Alisema vigezo wanavyotumika watoa huduma kupanga bei za huduma za mawasiliano ikiwemo data ni pamoja na gharama za uwekezaji na uendeshaji, idadi ya watoa huduma na muundo wa soko, Sera, Sheria na Kanuni zinazosimamia sekta, ukubwa wa nchi na upatikanaji wa rasilimali wezeshi za mawasiliano.
Dkt. Bakari ameongeza kuwa takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 95 ya watumiaji wa huduma za mawasiliano upendelea kutumia huduma za vifurushi kutokana na kuwa punguzo kubwa, hivyo kuweka unafuu katika matumizi ya huduma za mawasiliano.
Akitolea ufafanuzi changamoto suala la data kuisha haraka Dkt. Bakari alisema kwa mujibu wa utafiti waliofanya wamegundua kuwepo sababu mbalimbali zikiwemo kuongezeka kwa kasi ya mtandao na uwezo wa Simu-Janja, kuongezeka kwa ubora wa picha na video zinazojihuisha mara kwa mara bila mtumiaji kujua.
“TCRA imekuwa na utaratibu wa mara kwa mara kufanya stadi za bei za huduma za mawasiliano ambapo stadi ya sasa inaonesha kuwa, gharama halisi ya kuuza data nchini ni kati ya TZS 2.03/Mb hadi TZS 9.35/Mb. TZS 2.03/Mb ni bei ambayo mtoa huduma anaweza kuuza Data na kurudisha gharama zake za uendeshaji na TZS 9.35/Mb ni bei ambayo mtoa huduma anaweza kuuza data na kutoa huduma zenye ubora na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema Dkt. Bakari.
Dkt. Bakari aliongeza kuwa mujibu wa tafiti mbalimbali za bei za huduma za data, Tanzania kwa sasa ndiyo ina bei ya chini zaidi kwa Mb kwa nchi za Afrika Mashariki na SADC ambapo wastani wa gharama za data nchini ni takribani dola 0.75 za Kimarekani kwa Gb moja ya data sawa na shilingi za Kitanzania TZS 1,725 (sawa na TZS 1.68/Mb).
Aidha amebainisha kuwa kwa barani Afrika, Tanzania ni miongoni mwa nchi sita kati ya 52 zenye gharama nafuu za data.







