Breaking News

TANESCO KUTUMIA BILIONI 144 KUIMARISHA GRIDI YA TAIFA

Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) limesaini mkataba wa kuimarisha gridi ya Taifa wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 144 na Kampuni ya Grid Solutions kutoka nchini Ufaransa Juni 17, 2022. 

Akisaini mkataba huo Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Maharage Chande ametaja sehemu ya kwanza itahusisha kuboresha vituo tisa vya kupoza umeme vya gridi katika Maeneo ya Mlandizi, Chalinze, Same, Bukoba, Mbeya, Tabora, Mufindi, Musoma,na Mwanza.

Maharage ameainisha eneo lingine linahusisha kuimarisha mkonge wa mawasiliano ambao utaviwezesha vituo kuwasiliana na vituo vingine ndani ya nchi na Africa Mashariki

“Sehemu ya nyingine itakuwa kuboresha kituo cha kudhibiti mifumo ili kuendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwa wateja wetu,” amefafanua Maharage.

Amesema mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 21 na kugharimu trakribani shilingi bilioni 144.

"Kukamilika kwa mradi huu kutakuwa na manufaa makubwa kwa nchi na kwa wateja wetu kwani hali ya upatikanaji wa umeme itaimarika sana na kuongeza uwezo wa vituo hivyo kuhudumia wateja wengi zaidi," amesema Maharage.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Grid Solutions Benoit Pradairol ameishukuru TANESCO kwa kuwaamini na kuwapa kazi hiyo na wanatarajia kuifanya kwa ufanisi.

"Ni matumaini yetu mradi huu utakamilika ndani ya wakati na kufikia lengo la TANESCO," Alisema Benoit Pradairol.

Aidha, kukamailika kwa mradi huu kutaiwezesha TANESCO kupunguza upotevu wa mapato kwenye njia za usafirishaji na usambazaji wa umeme.