Breaking News

NAIBU WAZIRI FEDHA MHE. CHANDE AITAKA TRA KUTOA ELIMU YA KODI KWA WAFANYABIASHARA NA WAWEKEZAJI

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akifafanua jambo katika Mahafali ya Kumi na Sita ya Chuo cha Kodi yaliyofanyika katika ukumbi wa Multipurpose jijini Dar es Salaam

Dar es salaam:
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande amekitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara, na wawekezaji kwani wengi wamekuwa wakitumia wasaidizi wao kushughulikia masuala hayo kwa kukosa elimu hiyo.

Akizungumza katika mahafali ya kumi na sita ya Chuo Cha Kodi yaliyofanyika  chuoni hapo ambapo alikishauri chuo hicho pia kuanzishwa kozi fupi kwa wafanyabiashara ili kutatua changamoto za ulipaji kodi zinazotokana na wafanyabiashara kukosa elimu.

"Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakilalamikia mifumo ya ulipaji kodi kumbe tatizo ni kwamba hawana elimu, hivyo utoaji wa elimu ya kodi itasaidia kutatua changamoto hizo na kuondokana na malalamiko" alisema Mhe. Chande. 

Mheshimiwa Chande Amekipongeza chuo hicho kwa kuwa kituo cha umahiri wa mafunzo ya kodi na forodha kwa ukanda wa Afrika Mashariki na kukitaka kiongeze juhudi kifikie ubora kwa bara zima la Afrika.

Pia alikitaka chuo hicho kuongeza nguvu katika kufanya utafiti utakaosaidia kutatua changamoto za ukusanyaji kodi wa biashara za mtandaoni kwani bado hakuna mfumo mzuri wa ukusanyaji kodi wa biashara hizo.

Vile vile, aliwataka wahitimu kutumia taaluma yao kwa manufaa ya taifa kwa kutoa elimu ya kodi kwa wananchi na kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa weledi watakapoenda ili kukiwakilisha vyema chuo hicho.

Awali, akizungumza katika mahafali hayo Mkuu wa chuo hicho Profesa Isaya Gairo alisema kuwa chuo kinafanya maboresho ya mafunzo kidijitali kuendana na kasi ya teknolojia.

Alibainisha kuwa chuo kimeshaanza kuvhukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanza kwa ukarabati wa miundombinu ikiwemo jengo la utawala ambapo Waziri Chande aliahidi kuwa serikali itaendelea kutoa fedha kutimiza malengo ya kimkakati ya chuo.

Alisema udahili kwa wanafunzi ambao ni wafanyakazi wa TRA umekuwa ukiongezeka kila mwaka tangu Chuo kipate Ithibati mwaka 2007 udahili wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania umeongezeka kutoka wanafunzi 974 mwaka 2008/2009 hadi kufikia wanafunzi 1,766 mwaka 2022/2023.

"Chuo kimendelea kushirikiana  na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, ambapo kimehuisha makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Kodi-International Bureau of Fiscal Documentation (IBFD), na kuendeleza ushirikiano na Mtandao wa Kimataifa wa Vyuo Vikuu vinavyotoa mafunzo ya Forodha" Alisema Prof. Jairo

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Cha Kodi, Dkt. Samwel Werema, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya elimu nchini na kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi.

Dkt. Werema alisema kuwa Katika muktadha huo, Chuo kitaendelea kubuni mafunzo mbalimbali kwa ajili ya wadau wa Mamlaka ambayo yanaendana na matarajio ya Serikali pamoja na mabadiliko ya kiuchumi Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.