Breaking News

FURAHIKA EDUCATION YAPOKEA MIL 200 KUENDELEZA MRADI WA ELIMU BURE KWA VIJANA WALIOKOSA FURSA YA KUENDELEA NA MASOMO

Kaimu Mkuu wa Chuo cha FURAHIKA Education central Dokta David Msuya, akifafanua jambo wakati akizunguza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam. 

Dar es Salaam
Shirika la Furahika limepokea shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuendeleza mradi wake wa Elimu Bure kwa vijana ambao wamekosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kitokufaulu katika mitihani yao pamoja na ukatili wa kijinsia.

Akizungumza mapema leo 18 desemba 2023 makao makuu ya kituo hicho Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam Kaimu Mkuu Kituo 
hicho Dokta David Msuya amesema  kituo hicho kimesajiliwa usajili namba VET/DSM/PR/2021/D169 kwa lengo la kutoa fursa kwa vijana ambao wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufeli mitihani, kutokuwa na uwezo pamoja na ukatili wa kijinsia kuweza kupata fursa ya kujiendeleza kielemu. 

“Vijana tunaowapokea kwa ajili ya masomo ni wale walioshindwa kuendelea na shule kwa kupata alama hafifu katika  matokeo ya darasa la saba, kidato cha pili na nne ama kushindwa kulipa ada, hapa tunawakaribisha ili watimeze ndoto zao na kuepuka utegemezi,” Alisema Dkt. Msuya.

Alisema kituo kimekuwa kikiwapokea vijana kutoka maeneo mbalimbali na kuwasaidia kuwapa ujuzi wa fani mbalimbali ikiwemo kozi ya Utalii, Hotel Management, Ushonaji, IT na nyinginezo zitakazowasaidia kupata ajira ama kujiajiri wenyewe ambapo tunatarajia kuanzia Januari 2024 kituo katika kuhakikisha kinaboresha zaidi kinataji kuanza kufundisha kozi mpya ambazo watazitangaza.

"Kwasasa kituo kipo katika mchakato wa kupokea vijana kutoka maeneo mbalimbali na kuwasajili kwa ajili ya muhula mpya wa masomo zoezi litakalofanyika mpaka mwisho mwezi Janauri 28, 2024 hivyo napenda kutoa rai kwa wazazi ama walezi kutumia nafasi kwa kuwaleta vijana wao kupata elimu bure bila malipo" Alisema Msuya

Amefafanua kuwa chuo hicho kinafanya kazi zake kwa mujibu wa utekelezaji wa miradi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum kupitia Ustawi wa Jamii.

Kutokana na wiki hii kuwa ya kupinga vitendo vya ukatili, Dkt. Msuya ametoa wito kwa Serikali kuangalia namna ya kutunga sheria ya kuwadhibiti baadhi ya wazazi ama walezi wenye tabia ya kutumikisha watoto wakati wa muda wa masomo kwa kutembeza biashara kama mbogamboga, matunda n.k.

“Baadhi ya watoto utawaona wanatembeza biashara wakati wa masomo wenzao wakiwa darasani huo nao ni ukatili na unapaswa kukemewa na kuwachukulia hatua wazazi, walezi wanaokwepa majukumu yao ya kutafuta kipato kwa ajili ya familia badala yake wanawatumia watoto kubeba mzigo huo,” Alisema.

Aidha dkt. Msuya ametoa shukrani kwa wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakishirikiana na kituo hicho kwa kutoa nafasi kwa wahitimu wake hususani Mkurugezi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), bwama Masanja Kadogosa, kwa kuajili wahitimu kutoka chuo hicho katika fani za upishi katika mradi SGR katika kituo cha reli, Mlandizi