Breaking News

KILIO CHA BEI YA SUKARI NA NAULI ZA MABASI SERIKALI IWAFUTE MACHOZI WANANCH

Waziri Kivuli wa Uchukuzi Ndg. Kiza Mayeye akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya chama hicho leo 4 February 2024 Jijini Dar es salaam.

Waziri wa Viwanda na Biashara Ndg. Halima Nabalang’anya akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya chama hicho leo 4 February 2024 Jijini Dar es salaam.

Dar es salaam
Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuwafuta machozi wananchi kwa kusitisha nauli mpya za mabasi na daladala zilizoanza kutumika tangu mwezi Desemba 2023 na kuitaka Serikali ichukue hatua madhubuti kushusha bei ya sukari inayolalamikiwa na wananchi nchi nzima. 

Kauli hizo zimetolewa na Waziri Kivuli wa Uchukuzi Ndg. Kiza Mayeye na Waziri wa Viwanda na Biashara Ndg. Halima Nabalang’anya leo jumapili 4 February 2024 wakizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama. 

Kwa upande wa tatizo la ongezeko kubwa la nauli mpya za mabasi na daladala Waziri Kizza amesema bei mpya zilizotangazwa na Serikali zimeongezeka kwa wastani wa kati ya Shilingi 270 hadi shilingi 400 kwenye shilingi 1,000 kwa daladala. Kwa upande wa nauli za mabasi amesema ndio imeleta maumivu zaidi kuna mikoa imeongezeka Shilingi 6,000 hadi 17,000 wastani wa asilimia 18 hadi 22.

“Kitendo cha Serikali kuridhia maamuzi ya bodi ya LATRA inaonyesha wazi kabisa haiwajali wananchi wake na kuwatelekeza. Nauli hizi zimeangalia maslahi ya wasafirishaji na si hali za wananchi wa kawaida.” Ameongeza Kizza Mayeye. 

Aidha, Waziri Kizza ametoa wito kwa Serikali kusitisha matumizi ya nauli mpya ili kutoa nafasi kwa LATRA  kufanya marejeo upya na Serikali kufanyia kazi madai ya wasafirishaji kwa kurejesha ruzuku kwenye mafuta na matumizi ya Gesi asilia. 

Katika hatua nyingine kuhusu kupanda kwa bei ya sukari Waziri Kivuli wa Biashara na Viwanda amesema kauli za Serikali hazijasaidia hata kidogo kutoa nafuu ya bei ya sukari tofauti na ahadi na hadaa inazozitoa. Hivyo ameitaka Serikali kwa hatua za haraka iweke nguvu kubwa kuhakikikisha upatikanaji wa kutosha wa sukari ili kuhakikisha bei inashuka na wananchi wanapata sukari kwa wakati na kwa bei nzuri.

“Tunaitaka Serikali kuongeza kasi ya uwekezaji na uzalishaji katika viwanda kwa kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria na kuchochea matumizi ya teknolojia za kisasa.” Ameongeza zaidi.

Alisema chama cha ACT Wazalendo kitaendelea kusisitiza kuwa kazi kubwa ya Serikali yoyote ile dunia ni kuangalia ustawi wa wananchi wake. Kitendo cha Serikali kutumia hadaa na kuziba masikio juu ya kero za sukari na kupanda kwa nauli tena ndani ya miaka miwili mfululizo kutangazwa bei mpya mara mbili ni kuichora kama Serikali isiyojali.