DKT. RHIMO NYANSAHO AANZA RASMI MAJUKUMU KAMA MKURUGENZI MKUU WA PSSSF
Dodoma – Dokta Rhimo Nyansaho ameanza rasmi majukumu yake kama Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) baada ya kupokelewa katika Makao Makuu ya PSSSF jijini Dodoma.
Katika mapokezi hayo, Dkt. Nyansaho alipokelewa na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul-Razaq Badru, ambaye alimuongoza na kumtakia mafanikio katika majukumu yake mapya.
Uteuzi wa Dkt. Nyansaho ulifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 26 Mei mwaka huu.
Dkt. Nyansaho anatarajiwa kuendeleza jitihada za kuboresha huduma za hifadhi ya jamii na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu ya PSSSF kwa manufaa ya wanachama wake na Taifa kwa ujumla.




