Breaking News

NLD YAWAONYA WANACHAMA WAKE KUEPUKA VURUGU ZA JULAI 7

Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan, amewataka wanachama wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla kuepuka kujihusisha na vitendo vyovyote vya vurugu vinavyodaiwa kupangwa kufanyika Julai 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Julai 1, 2026, baada ya kikao cha Katibu Mkuu wa chama hicho, Doyo alisema viongozi na wanachama wa NLD wameazimia kutoshiriki wala kuunga mkono vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

"Katika kikao chetu cha Julai 1 na Julai 2, tumeazimia kutohusika na vurugu zozote zinazodaiwa kufanyika Julai 7 mwaka huu," alisema Doyo.

Aidha, aliwataka Watanzania kupuuza kauli zozote zinazoweza kuchochea taharuki au kuvuruga utulivu wa taifa, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda amani na mshikamano wa nchi.

Doyo alisema kikao hicho pia kilijadili hali ya kisiasa inayoendelea nchini pamoja na mikakati ya kuendelea kuimarisha chama ili kiweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi.