NEMC YATOA SIKU 90 KWA VITUO VYA AFYA NA HOSPITALI KUWEKA MIUNDOMBINU KUTEKETEZA TAKA
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limetoa siku 90 kwa taasisi zote zinazotoa huduma za afya nchini kuweka miundombinu ya kuteketeza taka au kuwapa wakandarasi waliothibitishwa kisheria kuepuka kuhatarisha afya na mazingira kwa ujumla.
Akizungumza jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Ufuatiliaji Sheria NEMC, bwana Hamad Taimuru amesema katika siku za h8vi karibuni kumekuepo na usafirishaji na utupaji taka hizo hovyo bila kufuata miongozo na kanuni zilizopo unaweza kuleta athari kubwa kwa mazingira, binadamu pamoja na wanyama ikiwemo kuzuka kwa magonjwa mbalimbali.
"Baadhi ya watoa huduma za afya wasio waaminifu ambao wanakiuka matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 na Kanuni zake kwa kusafirisha na kutupa taka zinazotokana na huduma za afya bila kufuata utaratibu uliowekwa na Sheria pamoja na Wizara ya Afya ama bila kuwa na vibali vya Wizara husika katika utekelezaji wa majukumu yao". Alisema Taimuru.
Alisema mara baada ya muda huo kupita NEMC watafanya ukaguzi katika vituo vya afya nchi nzima kuona utekelezaji wa agizo hilo na wale ambao watakaokiuka watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kusimamishwa kutoa huduma mpaka watakapotekeleza agizo hilo.
Aidha bw. Taimuru aliongeza kuwa Baraza linazielekeza Mamlaka za udhibiti nchini zinazoshughulika na usimamizi wa taka zinazozalishwa ma watoa huduma za afya nchini kuhakikisha wanafuata miongozo iliyowekwa na Wizara pamoja masharti ya Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa taka hatarishi za Mwaka, 2021 ikiwemo kuwa na miundombinu ya usimamizi wa taka zao pamoja na vibali vilivyotolewa na Wizara ya afya.
Alisema baraza linakemea tabia ya baadhi ya watoa huduma za afya kuwapa taka watu ambao hawajaidhinishwa kutoa huduma na kuzitupa hovyo jambo ambalo ni hatari kwa afya na mazingira.
"Baraza litaendelea kusimamia Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 kifungu cha 137 pamoja na kanuni za usimamizi wa taka hatarishi kanuni ya 52 mpaka 58 kwa kushirikiana na Mamlaka zote husika nchini kudhibiti ukikwaji huo wa Sheria. Kadhalika adhabu kali zitatolewa kwa wote ambao hawataweza kutekeleza agizo hili ikiwemo kufungiwa vituo vyao mpaka watakapoweka miundombinu madhubuti ya uhifadhi, usafirishaji na uteketezaji wa taka zao". Alisema Taimuru.




