SERIKALI YAWEKA MKAZO MASUALA YA USALAMA NA AFYA KAZINI
Dar es Salaam - Serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuimarisha usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini ili kulinda wafanyakazi pamoja na kuongeza tija katika uzalishaji.
Hayo yamesemwa, Aprili 23, 2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani ambapo amesema Serikali ilianzisha taasisi ya OSHA kwa lengo la kuhakikisha kuwa mazingira ya kazi yanakuwa salama, yenye kuzingatia viwango vya afya, na yanayopunguza ajali pamoja na magonjwa yatokanayo na kazi.
Waziri Sangu, amehimiza waajiri kuhakikisha wanatoa vifaa kinga, kuboresha miundombinu ya sehemu za kazi na kuweka mifumo madhubuti ya kushughulikia dharura. Kwa upande mwengine ametoa wito kwa wafanyakazi kufuata taratibu za usalama na kutoa taarifa mapema wanapobaini hatari zinazoweza kusababisha ajali au madhara kiafya.
Vile vile, amesema Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kama Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika kuboresha viwango vya usalama na afya kazini, sambamba na kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kazi.
Akizungumzia maadhimisho hayo kitaifa yatakayofanyika Aprili 28, 2026 mkoani Njombe, amesema yatalenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa usalama na afya kazini kupitia kauli Mbiu "Mazingira Bora ya kazi kisaikolojia ni Njia ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kujenga Taasisi imara.
Ameongeza kuwa katika maadhimisho hayo, Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendesha kampeni maalum za uhamasishaji kupitia mafunzo kwa makundi mbalimbali, ikiwemo wajasiriamali wadogo.
Kadhalika, Waziri Sangu amewaalika wananchi wa mkoani Njombe na maeneo ya jirani kutembelea na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kuanzia Aprili 24 hadi 29, 2026 katika viwanja vya Shule ya Mji Mwema, Mkoani Njombe,





