RAIS DKT. SAMIA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA MIAKA 20 YA BARAZA LA AMANI NA USALAMA LA UMOJA WA AFRIKA
Dar es salaam
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua kongamano la maadhimisho ya miaka 20 ya baraza la amani na usalama la umoja wa Afrika yatakayofanyika Mei 25, katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema ni heshima kubwa Tanzania kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo ambapo wageni 120 wanatarajiwa kuhudhuria kutoka nchi mbalimbali.
Amesema, Tanzania kuwa wenyeji wa maadhimisho hayo ni heshima kubwa kwani ni moja kati ya nchi 15 kati ya nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika, ambao ni wajumbe wanaounda baraza la amani na usalama la umoja wa Afrika.
"Nipende pia kuwataarifu kuwa pamoja na kuwa wajumbe, mwezi huu wa Mei 2024, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepewa jukumu jingine kubwa zaidi, tumeaminiwa kuwa Mwenyekiti wa baraza hili kwa mwezi Mei, hivyo, tukiwa wenyekiti tunalo jukumu kubwa la kusimamia shughuli zote zinahusu baraza, ikiwemo kufuatilia kwa karibu hali ya ulinzi na usalama kwenye bara la Afrika". Alisema Mhe. Makamba.
Aidha katika maadhimisho hayo Tanzania kwa kushirikiana na sekretarieti ya baraza hilo waliandaa ratiba ya shughuli mbalimbali ndani ya mwezi huo ambapo wiki ya kwanza itahusu usuluhishi na majadiliano, wiki ya pili ilihusu masuala ya mahitaji ya kibinadamu, amani na usalama, wiki ya tatu ilihusu wanawake na vijana katika amani na usalama na wiki ya nne ulinzi kwa watoto na wiki ya tano ilihusu kusaidia misheni za amani
Amesema maadhimisho hayo pia yataudhuliwa na vingozi mbalimbali wakiwepo wa marais waliopo madarakani, mawaziri, marais wastaafu na watu mashuhuri.
Amewataja baadhi ya viongozi mashuhuri watakaoshiriki maadhimisho hayo ni Mhe. Jessica Alupo, Makamu Rais wa Uganda; Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Olesegun Obasanjo, Rais Mstaafu Burundi, Mhe. Domitien Ndayizeye, Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Joachim Chissano na Mhe. Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
"Nchi ambazo zina wajumbe wa baraza hilo ni Tanzania, Uganda na Djibouti (kutoka Ukanda wa Mashariki), Cameroon, DRC na Equatorial Guinea (Kanda ya Kati), Afrika Kusini, Angola na Botswana (Kanda ya Kusini), Cote d’Ivoire, Gambia, Nigeria na Sierra Leone (Magharibi) na Misri na Morocco (Ukanda wa Kaskazini)". Alisema mhe.Makamba.




