Breaking News

TALGWU NAO WALAANI KAULI YA RC MAKONDA

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa nchini (TALGWU), kimemtaka mkuu mkoa wa Arusha Paul Makonda kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma pale anapozungumza na watumishi wa Umma na kuacha kutoa maneno ya kashfa na dhihaka kwa mtumishi iwe mbele ya hadhara au pasipo hadhara.

Kauli ya TALGWU inakuja kufuatia video fupi ikimuonesha Makonda akiwa kwenye mkutano wa hadhara huku akimuhoji mtumishi wa Umma katika ziara yake wilayani Longido Mkoani Arusha ambapo katika Video hiyo alionekana akitoa matamshi kwa mtumishi huyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano wa Kimataifa (TALGWU), Shani Kibwasali wakati akilaani matamshi aliyotoa mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa mtumishi huyo.

Kibwasali amesema TALGWU inatambua kazi kubwa anayofanya Makonda katika masuala mbalimbali ikiwemo kusimamia miradi ya maendeleo wanamsihi kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma.

“Mtumishi yule ni mwanachama wetu na kama chama hatuwezi hata kidogo kufumba macho pale ambapo mwanachama anafanyiwa vitendo ambavyo ni kinyume na sheria,kanuni,taratibu,miongozo na maadili ya Utumishi wa Umma”Amesema Kibwasali.

Aidha Kibwasali ametoa rai kwa Viongozi wote wa Serikali walioaminiwa na Rais katika kuhudumia na kuwaongoza watanzania kuacha mara moja kutumia dhamana walizopewa kwa kutoa maneno ya Kashfa kwa Wafanyakazi.

“Endapo mtumishi amekosea zipo taratibu za kiutumishi za kumchukulia hatua na sio kudhalilisha utu wake na kumvunjia heshima Mfanyakazi”