WANANCHI MTWARA WARIDHISHWA NA RIPOTI YA TUME YA RAIS, WASISITIZA MARIDHIANO YA KITAIFA
Wananchi wa mkoa wa Mtwara wameeleza kuridhishwa kwao na mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Rais ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Wakizungumza kufuatia uwasilishwaji wa ripoti hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam, wananchi hao wamesema kuwa ripoti hiyo imezingatia maoni halali ya Watanzania wengi, hivyo kuwa msingi muhimu wa kuimarisha hali ya kisiasa na kijamii nchini.
Aidha, wamepongeza juhudi za tume hiyo kwa kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha mapendekezo wanayoamini yanaweza kusaidia kuzuia matukio kama hayo kujirudia siku zijazo.
Wananchi hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa maridhiano ya kitaifa, wakieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda na kuendeleza misingi ya amani, umoja na mshikamano uliopo nchini.
“Nitoe rai kwa Watanzania kuunga mkono mapendekezo yote yaliyotolewa na tume, ikiwemo suala la maridhiano ya kitaifa, pamoja na kuendelea kulinda na kudumisha amani, umoja na mshikamano tulionao nchini,” amesema mmoja wa wananchi hao.
Kwa ujumla, wameitaka jamii kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa mapendekezo hayo ili kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na utulivu na maendeleo endelevu.




