Breaking News

JESHI LA POLISI: HALI YA USALAMA NI SHWARI, WATU 37 KWA MAKOSA YA MTANDAO

Hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam imeelezwa kuwa shwari, huku Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam likiendelea kuimarisha ulinzi kupitia ushirikiano na wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Aprili 20, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Muliro Jumanne Muliro, amesema kuwa katika eneo la Ubungo, watu 37 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya kimtandao, yakiwemo kutoa vitisho na kutumia lugha za matusi dhidi ya watu mbalimbali.

Ameeleza kuwa baadhi ya watuhumiwa hao ni wafanyakazi wa kampuni za INNOVIX CALL CO LTD na OTAIGO Financial Services Company Limited, zinazojihusisha na utoaji wa mikopo kwa njia ya mtandao.

Miongoni mwa watuhumiwa waliotajwa ni Renatus Mujwahuzi maarufu kama “Migeyo” mkazi wa Mbezi Beach, Odilia Oswin “Ngunga” mkazi wa Goba Njia Nne, na Theresia Brastius “Kanu” mkazi wa Mtoni Kijichi. Watuhumiwa wengine 34 wanaendelea kuchunguzwa.

Kamanda Muliro amesema hatua zinaendelea kuchukuliwa ili kuwafikisha watuhumiwa hao katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limeeleza mafanikio ya utekelezaji wa mifumo ya haki jinai kwa kipindi cha Machi hadi Aprili 2026, ambapo watuhumiwa kadhaa wamefikishwa mahakamani na kupatikana na hatia kwa makosa mbalimbali mazito.

Miongoni mwa waliohukumiwa ni Hashimu Kasimu “Duma” mkazi wa Kimara, aliyepata kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kulawiti na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo. Pia, Vicent Laurent “Ndimbo” mkazi wa Urafiki Kinondoni alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kwa kosa la kubaka.

Wengine ni Habibu Nassoro mkazi wa Charambe aliyepata kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti, pamoja na Ismail Ally “Muro” aliyepata kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka, wote wakihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Temeke.

Katika kesi nyingine, Nelson Julius mkazi wa Mavurunza Kimara alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Aidha, Fadhili Issa, Peniel Jonathan “Mtakibaleza” na Yusuph Iddi, wote wakazi wa Mbagala, walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa ya kubaka, huku Yusuph Iddi akikutwa na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi.

Jeshi la Polisi limetoa shukrani kwa wananchi kwa kuendelea kushirikiana nao kwa kutoa taarifa zinazosaidia kudhibiti uhalifu. Aidha, limehimiza jamii kuendeleza ushirikiano huo kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na kujitokeza mahakamani kutoa ushahidi ili kusaidia haki kutendeka.

Polisi imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia kikamilifu sheria na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaimarika siku hadi siku.