HALI SIO SHWARI NDANI YA HIFADHI YA NGORONGORO, WANYAMA WAENDELEA KUWA TISHIO.
Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lilianzishwa mwaka 1959 likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 8,292, wananchi takribani 8,000 na mifugo isiyozidi 260,000. Kwa sasa eneo hilo idadi ya wananchi inakadiriwa kufikia zaidi ya 110,000, mifugo zaidi ya laki 8, idadi kubwa ya wanyamapori na shughuli zingine za kibinadamu huku eneo likibaki na ukubwa uleule.
Katika eneo hili kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanyamapri ambapo kwa mara kadhaa wamekuwa wakifanya mauaji ya wananchi na kwa mujibu wa takwimu kwa takribani katika kipindi cha miaka sita watu 68 wameshapoteza maisha yao na wengine 223 kujeruhiwa.
Matukio haya ya wananchi kushambuliwa na wanyama pori yanatokana na sababu ongezeko la wanyama hao ambapo kwa sasa wamekuwa wakihatarisha ustawi wa wananchi pamoja na mifugo yao.
Hali hii inaathiri maisha ya wananchi na kuongezeka migongano baina yao na wanyamapori ambapo hadi sasa wananchi kadhaa wameuliwa au kujeruhiwa endelea ambapo wanyama ambao wamekuwa wakisumbua sana wananchi simba, tembo, Nyati, fisi na viboko.
Kwa mujibu wa Afisa Tarafa ya Ngorongoro, Bw. Bahati Mfungo anasema kuwa hali ya wananchi kuuliwa na kushambuliwa na wanyama pori imeifanya serikali kufanya maamuzi ya kuwahamasisha wananchi hao kuhamia katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine ili pamoja na mambo mengine kuwanusuru na kuboresha maisha yao.
“Kinachotokea ni kwamba idadi ya watu imekuwa ikiongezeka na wanyamapori nao wamekuwa wakiongezeka hivyo kuwepo na hali ya kugombania eneo baina ya binadamu na wanyama jambo ambalo limekuwa likiwafanya wananchi katika eneo hili waishi katika mazingira magumu” alisema Bw. Mfungo.
Afisa tarafa huyo aliongeza kuwa jambo la msingi kwa sasa ni kwa wananchi kuitikia wito wa serikali wa kuhama katika eneo hilo ili kuokoa maisha yao kwani mamlaka zimekuwa zikithamini uhai wa wananchi na hivyo kutafuta njia ambazo zitaokoa maisha yao.
Matukio haya yameleta hofu na taharuki miongoni mwa jamii za wenyeji, wengi wakihofia usalama wao na wafamilia zao huku wengine wakikiri kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la Wanyama pori hifadhini hata kufikia hatua ya kuwa karibu na makaazi ya watu.
Bw. Kambatai Liariti Orkedienye (32) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Bulati, kata ya Nainokanoka, Tarafa ya Ngorongoro ni mmoja wa wahanga wa matukio ya kujeruhiwa na wanyama yaliyotokea hivi karibuni ndani ya Hifadhi.
Akizungumzia tukio hilo la kusikitisha, Bw. Kambatai alisema kwamba ilikuwa ni siku ya jumanne tarehe 9/7/2024 majira ya saa 3:00 asubuhi ambapo kama ilivyo ratiba yake ya kila siku, aliamka na kwenda kuchunga maeneo ya Embakai kreta na akiwa huko ghafla ng’ombe wake walivamiwa na simba wawili na baada ya kusikia kelele za ng’ombe alisogea na ndipo hapo simba mmoja alimwona na kumvamia.
“Niliposikia kelele za ng’ombe nilisogea na kuwaona simba wawili wakiwa wamewavamia ng’ombe na hapo hapo simba mmoja alinikimbilia na kunijeruhi mkono na kwenye mbavu nilidondoka chini na sikuweza tena kuelewa chochote baada ya hapo nilipoteza fahamu na baadaye nilijikuta nipo hospitali”. alisema Bw. Kambatai.
Tukio hili ambalo kwa kiasi kikubwa limewasikitisha wengi kijijini hapo, halikuwa tukio pekee kuna matukio mengine ambayo yameripotiwa kutokea likiwemo la mzee Melau Olenjoni aliyekuwa na umri wa miaka 60 kutoka Kijiji cha Nainokanoka aliyeshambuliwa na simba usiku wa tarehe 4/5/2024 na kupoteza maisha yake huku akiwaacha wajane wawili na watoto 10.
Haya ni baadhi tu ya matukio yaliyoripotiwa kati ya mengi ambayo yamekuwa yakitokea ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, usalama wa wananchi wanaoishi Hifadhini umekuwa hatarini kutokana na ongezeko la wanyama ndani ya Hifadhi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya watendaji wa kijiji kwenye tarafa hiyo wanasema kwamba matukio ya watu kuuawa ama kujeruhiwa yamekuwa yakitokea mara kwa mara lakini wananchi wengi wamekuwa hawatoi taarifa polisi na katika vyombo vingine vya usalama.
Afisa Tarafa ya Ngorongoro Bw. Bahati Mfungo amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwaelimisha wananchi wa tarafa hiyo ili waweze kuhama katika tukio hilo na kwenda maeneo mengine kwa ajili ya kuboresha maisha na kunusuru uhai wa wananchi hao.
Mpango wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuwaelimisha wananchi hao ili waweze kuhama na kuhamia maeneo mengine ambapo inakadiriwa kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu idadi kubwa ya wananchi watakuwa wamefikiwa.




