Breaking News

HESLB NA NIDA WAINGIA MAKUBALIANO KUTUMIA (NIN) KATIKA MCHAKATO WA MIKOPO ELIMU YA JUU

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, akizungumza wakati wa uzinduzi wa makubaliano ya matumizi ya Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) kati ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na NIDA, uliofanyika mapema leo Mei 15, 2025, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa makubaliano ya matumizi ya Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) kati ya HESLB na NIDA, uliofanyika Mei 15, 2025, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam: Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wameingia makubaliano ya kutumia Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) kama sharti la lazima kwa wanafunzi wanaoomba mikopo kuanzia mwaka wa masomo 2025/2026.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi za waombaji wa mikopo ili kuboresha huduma na ufanisi wa kazi za Bodi.

“Kuanzia mwaka huu wa masomo 2025/2026, namba ya utambulisho (NIN) itakuwa hitaji la lazima kwa kila muombaji wa mkopo kupitia mifumo yetu. Tayari tumeunganisha mifumo yetu na ya NIDA ili kuhakikisha taarifa zinasomeka moja kwa moja,” amesema Dkt. Kiwia.

Dkt. Kiwia amewashauri waombaji wa mikopo kuhakikisha wanakuwa tayari na NIN mapema kabla ya dirisha la maombi kufunguliwa, na kusisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia pia katika ufuatiliaji na ukusanyaji wa mikopo kwa wanufaika waliomaliza masomo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Bw. James Kaji, amesema Serikali inalenga kuhakikisha kila mwanafunzi aliyemaliza elimu ya sekondari na mwenye umri wa kuanzia miaka 18, anasajiliwa na kupatiwa NIN na Kitambulisho cha Taifa ili kuwezesha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo mikopo ya elimu ya juu.

“NIDA imejipanga kutoa huduma bora na kwa wakati kwa kushirikiana na HESLB. Tunawaomba wanafunzi wajitokeze mapema kujisajili, badala ya kusubiri hadi wakati wa udahili au ajira ambapo hutokea msongamano mkubwa,” amesema Bw. Kaji.

Hatua hii ya HESLB na NIDA inalenga kuimarisha mfumo wa utoaji wa mikopo kwa kutumia teknolojia na taarifa sahihi za utambulisho wa kitaifa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha huduma kwa vijana wanaoendelea na masomo ya juu.