Breaking News

ADO SHAIBU: HAKUNA MWENYE HATI MILIKI YA KUGOMBEA NDANI YA ACT WAZALENDO

Songwe - Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza kwa msimamo thabiti kuwa kitaendelea kusimamia demokrasia ya kweli katika mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

Akizungumza katika maadhimisho ya Songwe Day yaliyowakutanisha watia nia wa nafasi za Ubunge na Udiwani kutoka majimbo yote ya Mkoa wa Songwe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ndugu Ado Shaibu, alieleza kuwa hadi sasa jumla ya watia nia wanane wa Ubunge wamejitokeza na kuchukua fomu kuomba ridhaa ya chama.

Miongoni mwa waliochukua fomu ni Peter Kayuni (Vwawa), Michael Nyilawila (Songwe), Himid Siwale (Momba), Ezekia Zambi, Nestory Viniwa Arusha na Emanuel Kalinga (Mbozi)
Ndugu Ado alisisitiza kuwa kwa mujibu wa taratibu za ACT Wazalendo, kila mwanachama mwenye sifa ana haki ya kugombea nafasi yoyote bila kujali cheo au umaarufu wake ndani ya chama.

“Sisi ACT Wazalendo tunaamini kuwa kama unahubiri demokrasia, lazima uianze ndani ya chama. Ndiyo maana kwa kila nafasi Urais, Ubunge, Ubunge wa Viti Maalum, Udiwani na Udiwani wa Viti Maalum kila mwanachama mwenye sifa ana haki ya kugombea. Hakuna mwenye hati miliki ya kugombea,” alisema Ndugu Ado.
Alionya pia kuwa chama hakitasita kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa viongozi wa ngazi za kata na majimbo watakaoweka vikwazo kwa watia nia kuchukua fomu za kugombea.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa ACT Wazalendo linaendelea na maandalizi ya uchaguzi sambamba na kusisitiza haja ya mageuzi ya msingi katika mfumo wa uchaguzi nchini.
Alibainisha maeneo sita muhimu ambayo chama hicho kinapigania yafanyiwe mageuzi:

1.Wakurugenzi wa Halmashauri kutopewa jukumu la kusimamia uchaguzi

2. Kuteuliwa kwa wajumbe wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria

3. Kukomesha uwepo wa kura feki

4. Kuzuia kuenguliwa kwa wagombea kiholela

5. Vyombo vya ulinzi na usalama kutoshiriki hujuma katika uchaguzi

6. Kuwalinda mawakala wa vyama dhidi ya bughudha na uingiliaji vituoni

Leo tarehe 16 Mei 2025, Ndugu Ado Shaibu anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Mbeya, ambako anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mbeya Day tukio litakalowakutanisha watia nia wa nafasi za Ubunge na Udiwani kutoka majimbo yote ya mkoa huo.