MATEMBEZI YA SAMIA FIRST TIME VOTERS MAMIA YA VIJANA WAJITOKEZA
Arusha: Maelfu ya vijana kutoka vyuo na taasisi za elimu ya juu mkoani Arusha wamejitokeza kwa wingi kushiriki katika matembezi ya amani yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaunga mkono First Time Voters na kuonesha mshikamano na juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Matembezi hayo yaliyofanyika jijini Arusha yameelezwa kuwa na lengo la kuhamasisha ushiriki wa vijana katika masuala ya kijamii na kisiasa, sambamba na kutambua mchango mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya elimu, hasa kupitia ongezeko la mikopo ya wanafunzi na maboresho ya mazingira ya kujifunzia.
Mgeni rasmi katika tukio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Ndugu Jokate Mwegelo, aliwahimiza vijana kuendelea kuwa walinzi wa amani na kuchangamkia fursa za uongozi wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
“Ni wakati wa vijana kuamka na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika maeneo yenu. Amani ni msingi wa maendeleo, hivyo tuitunze na tuwe sehemu ya maamuzi kwa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ujao,” alisema Jokate.
Vijana waliopata fursa ya kushiriki katika matembezi hayo walieleza kuridhishwa kwao na juhudi za serikali katika kuwajali na kuwawezesha kielimu, wakisema wamehamasika kujiandikisha na kushiriki uchaguzi kama wapiga kura kwa mara ya kwanza.
Tukio hilo limeacha gumzo jijini Arusha na kuonesha nguvu ya vijana katika kuchochea maendeleo na kulinda misingi ya demokrasia nchini.






