Breaking News

ZITTO KABWE AMJIBU HARBINGER SETHI (SINGA SINGA) SAKATA LA IPTL

Dar es Salaam – Kiongozi mkuu mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo ambae alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati wa sakata la IPTL, Zitto Kabwe amejibu tuhuma za kashfa zilizofunguliwa dhidi yake na Mfanyabiashara Harbinder Singh Sethi kuhusiana na sakata tata la IPTL. 

Akizungumza mapema leo Mei 18, 2025 amesema katika kipindi chote cha sakata hilo ajawahi kutamka uongo wala kumkashifu Bw. Sethi, bali amesema ukweli kwa nia ya kulitetea Taifa dhidi ya uporaji wa rasilimali.

Amesema maneno aliyoyasema na kuyaandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa X (zamani Twitter) ni ya kweli na yanatokana na nyaraka rasmi na maamuzi ya Mahakama ndani na nje ya nchi. 

“Nilizungumza kwa nia njema na kwa kwa mapenzi mema kwa nchi nikitumia nafasi niliyokuwa nayo kipindi hicho kama Mwenyekiti wa PAC kushughulikia sakata la Escrow,” alisema Zitto

Ametaja mambo matano ya Msingi ambayo nilisema na kuhoji kipindi chote cha sakata hilo kuwa ni:

1. Umiliki Tatanishi wa IPTL: Alieleza kuwa PAP, kampuni inayohusishwa na Bw. Sethi, haikuwahi kununua kihalali hisa za Mechmar zilizokuwa IPTL, na kwamba Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong ndiyo wamiliki halali wa hisa hizo.

2. Fedha za Escrow: Alidai kuwa PAP ilipokea fedha kutoka akaunti ya Escrow kwa kutumia nyaraka na mchakato uliojaa utata na udanganyifu, kisha kutumia sehemu ya fedha hizo kununua hisa za VIP Engineering.

3. Maamuzi ya Mahakama: Aliyataja maamuzi kadhaa ya Mahakama za ndani na nje ya nchi yaliyoonyesha kuwa PAP si mmiliki halali wa IPTL. Alisema Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilishafuta amri zote zilizompa PAP uhalali wa kumiliki IPTL.

4. Makubaliano na Serikali: Alifafanua kuwa Bw. Sethi alikubali makosa kupitia makubaliano ya “plea bargain” na Serikali na akalipa sehemu ya fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 26, lakini hadi sasa hajalipa salio.

5. Hatari kwa Taifa: Aliongeza kuwa licha ya maamuzi hayo yote, Bw. Sethi ameendelea kufanya mabadiliko ya bodi na umiliki wa IPTL kupitia kampuni ya Karenga Pty Ltd inayomilikiwa na familia yake, jambo linaloibua maswali kuhusu dhamira yake.

Aidha Zitto pia ametumia mkutano huo kutoa wiito kwa Umma na Vyombo vya Habari kufuatilia kesi hiyo mahakamani ili wapate ukweli kuhusu namna Bw. Sethi alivyojipatia mali za umma kwa njia ya utata kwani kuzungumza ukweli huu siyo kashfa bali ni wajibu wa kizalendo.

“Mwizi kuitwa mwizi si tusi, bali ni sifa yake. Hatutakubali kuendelea kunyonywa kupitia ujanja ujanja wa kisheria,” alisema Zitto