MWANDISHI RAHEL PALLANGYO ACHAGULIWA KUWA MJUMBE MKUTANO MKUU TFF KUPITIA FRAT
TANGA — Mwandishi wa michezo wa gazeti la HabariLEO, Rahel Pallangyo, amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT), katika uchaguzi mkuu uliofanyika leo jijini Tanga.
Katika uchaguzi huo, Rahel alimbwaga aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, Allanus Lwena, na kujipatia ushindi uliompa tiketi ya kuingia kwenye mkutano mkuu wa TFF kwa kipindi kijacho.
Katika nafasi ya Mwenyekiti, Emanuel Chaula alichaguliwa kuongoza FRAT, huku Maulid Mwikalo na Jovin Ndimbo wakichaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Aidha, mara baada ya uchaguzi, Mwenyekiti mpya Chaula alimteua Michael Kassanga kuwa Makamu Mwenyekiti, uteuzi unaoendana na matakwa ya katiba ya FRAT inayoruhusu uteuzi wa wajumbe watano kuingia kwenye Kamati ya Utendaji.
Akizungumza mara baada ya kutangaza matokeo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili George Banoba, aliwataka viongozi waliochaguliwa kuzingatia katiba na miongozo ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT), FRAT na TFF katika kutekeleza majukumu yao.
"Mliochaguliwa wote mmeapishwa kulinda katiba na miongozo ya BMT, FRAT na TFF, hivyo katekelezeni majukumu yenu kwa uadilifu," alisema Wakili Banoba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Chaula aliwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kuwaahidi kuwatumikia kwa bidii katika kipindi chake cha uongozi.




