Breaking News

PROF MBARAWA: NIT YAPATA ITHIBATI YA EASA KUWA KITUO CHA MITIHANI YA LESENI ZA KIMATAIFA ZA UHANDISI WA MATENGENEZO YA NDEGE

Na Mwandishi Wetu, Dodoma - Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ametangaza kuwa Serikali kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kwa kushirikiana na Athens Aviation Training Organization ya Ugiriki, imepata ithibati kutoka Wakala wa Usalama wa Anga wa Ulaya (European Aviation Safety Agency - EASA) kuwa Kituo cha Mitihani ya Leseni za Kimataifa kwa Wahandisi wa Matengenezo ya Ndege (EASA Part–66 Aircraft Maintenance License Training).

Akizungumza leo Alhamisi, Mei 15, 2025, bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/26, Profesa Mbarawa alisema kuwa NIT pia kitakuwa Kituo cha Mafunzo ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege (EASA Part–147 Maintenance Training Organization).

“Mafanikio haya ni ya kipekee kwa nchi yetu na yatawezesha wataalam wetu kuwa na ubora unaokidhi ushindani katika soko la ajira la kikanda na kimataifa,” alisema Profesa Mbarawa.

Aidha, alieleza kuwa Serikali kupitia NIT imepata ithibati ya kuanza mafunzo ya urubani kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ambapo mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza rasmi mwezi Juni 2025.

Kuhusu maendeleo ya jumla, Profesa Mbarawa alieleza kuwa NIT inaendelea kutoa kozi ndefu 48 za kimkakati kwa lengo la kuzalisha wataalam mahiri kwa ajili ya kuendeleza miradi mikubwa ya kitaifa. Kwa sasa, chuo kina jumla ya wanafunzi 17,701 ikilinganishwa na 16,131 kwa mwaka 2023/24, sawa na ongezeko la asilimia 9.7.

Akizungumzia miradi ya kimkakati, Waziri alibainisha kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu na vifaa vya kufundishia chuoni hapo, ikiwa ni pamoja na uundwaji wa ndege moja yenye injini mbili kwa ajili ya kufundishia marubani. Ndege hiyo inatengenezwa Marekani na inatarajiwa kuwasili mwezi Oktoba 2025.

Pia, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuanzisha Kampasi ya NIT mkoani Lindi kwa ajili ya kuendeleza rasilimaliwatu katika sekta ya usafiri majini, mafuta na gesi.

Waziri Mbarawa alieleza kuwa NIT inaendelea kuanzisha Kituo cha Umahiri kwa Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji kupitia mradi wa EASTRIP (East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project), ambapo ujenzi wa majengo matano katika Kampasi ya Mabibo, Dar es Salaam unaendelea. Mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,504 yamekamilika, huku majengo mengine matatu yaliyobeba madarasa 10, maabara 15, karakana tano na ofisi 25 yakiwa yamekamilika kwa asilimia 96.

Aidha, ujenzi wa jengo la karakana ya matengenezo ya ndege (Aviation Hangar) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) upo kwenye hatua ya kumpata mkandarasi. Hangar hiyo itatumika kuhifadhi ndege za mafunzo na kutolea mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege.

Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, vifaa vya mafunzo ya urubani na uhandisi wa matengenezo ya ndege tayari vimenunuliwa kwa asilimia 70, ikiwa ni pamoja na Flight Simulators mbili na programu mbalimbali za kompyuta kwa ajili ya maabara, madarasa na ofisi katika Kampasi ya NIT Mabibo na KIA.