Breaking News

WIZARA YA UCHUKUZI YAOMBA TRILLION 2.74 KWA BAJETI YA 2025/26

Dodoma - Waziri wa Uchukuzi nchini Tanzania Prof. Makame Mbarawa leo tarehe 15 Alhamisi 2025, ameliomba Bunge la Tanzania kuidhinisha Jumla ya Shilingi Trilioni mbili, Bilioni mia saba arobaini na sita, Milioni mia nne themanini na tano na kumi na nane elfu (2,746,485,018,000) kwaajili ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/26.

"Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ya Uchukuzi inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 2,746,485,018,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 125,438,950,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 2,621,046,068,000 ni kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo." Amesema Prof. Mbarawa.

Katika hotuba yake kwa Bunge wakati akiwasilisha Bajeti ya wizara hiyo, Waziri Mbarawa ameeleza kuwa kwa mwaka ujao wa serikali, Wizara yake itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele vyake vya kuendele,a ujenzi wa reli ya kisasa SGR katika ushoroba wa kati, kununua vitendea kazi pamoja na kuboresha reli zilizopo.

Aidha Wizara hiyo pia imepanga kuendeleza maboresho ya kampuni ya ndege Tanzania ATCL, Kuboresha miundombinu na huduma za bandari, kuimarisha usalama wa mawasiliano kwenye usafiri na usafirishaji kwenye Maziwa Makuu, uendelezaji na uendeshaji wa viwanja vya ndege pamoja na kuendeleza ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli zilizopo.

Aidha pia Wizara imeeleza kuwa itaendeleza miradi ya kielelezo ikiwa ni pamoja na Mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege Mwanza, Mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege Arusha, mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege Mtwara, Mradi wa ukarabati kiwanja cha ndege Kilimanjaro, Mradi wa uendelezaji wa viwanja vya ndege vya Mikoa pamoja na mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege Bukoba mkoani Kagera.