Breaking News

RAIS SAMIA: NIMEONA CLIP KADHAA ZA KUNISEMA

Dar es Salaam — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, amezitaka Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka dhidi ya wale wanaotumia mitandao ya kijamii na teknolojia kwa njia zisizofaa.

Akizungumza leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Rais Samia amekemea ongezeko la wanaharakati kutoka nje ya nchi wanaojaribu kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu wa taifa.

"Nimeona clip kadhaa za kunisema, mara nina ubaguzi na nini! Ninalofanya ni kulinda nchi yangu na ndiyo wajibu wangu niliopewa. Kwa hiyo hatutatoa nafasi kwa kiumbe yeyote kuja kutuvuruga hapa, awe wa ndani au kutoka nje," amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amezitaka wizara na maafisa husika kutoa ufafanuzi wa haraka kuhusu tuhuma na madai mbalimbali yanayoibuliwa na wanaharakati na watu wengine, ama kuyakanusha endapo si ya kweli, au kuchukua hatua stahiki iwapo yana mashiko katika sekta zao.

Rais Samia amesisitiza kuwa usalama wa taifa ni jukumu la pamoja na haipaswi kuruhusu mtu yeyote, kutoka ndani au nje, kuleta chokochoko zinazoweza kuhatarisha hali ya utulivu na mshikamano wa kitaifa.