RASMI MFUMO WA USAJILI WA WAANDISHI WAANZA, WENYE VYETI FEKI WAONYWA
Dar es Salaam - Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imefungua rasmi mfumo wa usajili wa Waandishi wa Habari kupitia tovuti ya https://taihabari.go.tz kwa ajili ya kuomba kuthibitishwa na kupatiwa Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Card).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika ofisi za Bodi zilizopo Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Ndg. Tido Mhando, alitoa onyo kali kwa watu watakaotumia vyeti visivyo halali wakati wa kujaza taarifa zao katika mfumo huo.
“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, Bodi hii itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya kidijitali. Maombi ya ithibati yatafanyika kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari,” alisema Mhando.
Mhando alieleza kuwa waombaji wanapaswa kuandaa mahitaji muhimu ikiwemo namba ya simu na barua pepe vinavyofanya kazi, picha ndogo ya pasipoti, barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri au kwa mwandishi wa kujitegemea (Freelancer), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), pamoja na ada ya ithibati ya shilingi 50,000.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuwasilisha vyeti vya elimu vilivyoskaniwa kwa mfumo wa PDF na kuthibitishwa na mamlaka husika ikiwa ni TCU kwa vyuo vikuu na NACTVET kwa vyuo vya kati. Alionya vikali dhidi ya uwasilishaji wa vyeti bandia, akisema ni kosa la kimaadili na kisheria.
“Usiweke cheti feki. Hili ni kosa linalokiuka maadili ya taaluma ya habari na pia linaadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi,” alionya.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, alieleza kuwa muda uliotolewa kwa watu waliokuwa kwenye tasnia hiyo bila sifa za kitaaluma ili wakasome na kutimiza vigezo ulikuwa ni miaka mitano, na baadaye kuongezewa mwaka mmoja na Waziri. Hadi sasa, jumla ya miaka nane imepita na hakutakuwa na nyongeza ya muda tena.
JAB imetoa wito kwa Wahariri, Waandishi na wadau wote wa habari wakiwemo waajiri, kushirikiana kikamilifu na Bodi hiyo katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari, maadili, uwajibikaji na weledi nchini.




