Breaking News

TEF WAANDISHI WA HABARI KUWENI NA ALAMA ZA VITAMBUZI WAKATI WA KURIPOTI KESI YA LISSU

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akizungumza na waandishi wa habari juu ya hatua wanazotakiwa kuchukua wakati wa kuripoti kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu mkutano uliofanyika makao makuu ya Jukwaa la wahariri (TEF) Jijini Dar es salaam 
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Dar es Salaam, Bakari Kimwanga akifafanua jambo katika mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Jukwaa la wahariri (TEF) Jijini Dar es salaam.


Dar es salaam - Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameshauri waandishi wa habari kuwa na alama za utambuzi wakati wa kuripoti kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 2 Mei 2025, katika ofisi ya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam alisema, miongoni mwa alama hizo ni kuvaa jaketi la uandishi wa habari na kitambulisho cha kazi.

"Baada ya zile purukushani pale mahakamani, nikasema haiwezekani mwandishi akazuiwa kufanya kazi yake.

"Nilikutana na Afande Jumanne Muliro (Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam) na tukakubalia kuzuia waandishi Kisutu sio jambo jema. Tukakubaliana siku ya kesi ya Lissu tarehe 6 Mei waingie wote lakini kuwe na utambuzi," alisema Bw. Balile

Balile alisema, mwandishi hapaswi kuzuiwa kufanya kazi yake ya kukusanya, kuchakata na kuhabarisha umma.

Hata hivyo alisema, wanahabari wanapaswa kufika mahakamani mapema kwa kuwa, chumba kikijaa hawatopata nafasi.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Dar es Salaam, Bakari Kimwanga alisema, wanahabari wanapaswa kuhakikisha wanakuwa salama wakati wa kazi.

"Jambo la usalama ni la kwanza kisha kazi (habari), jukumu la usalama ni lako mwanahabari," alisema Bw  kimwanga.