Breaking News

SERIKALI YAWATAKA WAHITIMU KIDATO CHA NNE 2025 KUBORESHA MACHAGUO KUPITIA MFUMO WA SELFORM KABLA YA MEI 10

Serikali imewataka wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka 2025 kutumia kikamilifu fursa ya kubadilisha machaguo ya tahasusi na kozi kupitia mfumo wa mtandao wa Selform, zoezi linaloanza rasmi Aprili 11 hadi Mei 10, 2026.

Akizungumza leo Aprili 11, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, amesema muda uliotolewa. unatosha kwa kila mhitimu kufanya marekebisho sahihi ya machaguo yao, huku akisisitiza kuwa kuchelewa au kushindwa kufanya mabadiliko kunaweza kusababisha changamoto baada ya matokeo kutangazwa.

Amesema wahitimu wanapaswa kutafuta ushauri wa kitaaluma kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au kozi ili kuhakikisha maamuzi yao yanaendana na uwezo wao na matokeo ya mtihani wa taifa.

Ameongeza kuwa baada ya dirisha la marekebisho kufungwa hakutakuwa na nafasi ya kushughulikia malalamiko yoyote yatakayohusiana na machaguo, hivyo ni muhimu kwa wahusika kuzingatia muda uliopangwa.

Aidha, huduma ya kubadilisha machaguo imetolewa bure, huku wanafunzi wakihimizwa kutumia dawati la huduma kwa wateja endapo watakumbana na changamoto katika mfumo huo.