Breaking News

UCSAF YATANGAZA MAFANIKIO MAKUBWA KATIKA KUKUZA SEKTA YA TEHAMA NA MAENDELEO YA MAWASILIANO NCHINI

Dar es Salaam, Mei 26, 2025 – Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umetangaza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kukuza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini, hususan kwa watoto wa kike, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya sayansi na teknolojia.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda, alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, mafunzo ya TEHAMA kwa wanafunzi wa kike yalifanyika mwezi Aprili na kuwahusisha takribani wanafunzi 248. Mafunzo haya yamelenga kuwahamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi.

Aidha, Mhandisi Mwasalyanga alieleza kuwa UCSAF imepeleka vifaa vya TEHAMA katika shule 22 za watoto wenye mahitaji maalum. Vifaa hivyo ni pamoja na mashine za kisasa za kusoma maandishi (readers), kompyuta mpakato (laptops), mashine za kuchapa nukta nundu (embossers na braille machines), Orbit Reader, rekoda za sauti (digital voice recorders), televisheni, na vifaa vya kukuza maandishi (magnifiers).
Katika kuboresha uwezo wa walimu, UCSAF imeendesha mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 3,180 katika taasisi za DIT, UDOM, na MUST. Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, walimu 3,798 kutoka shule 1,791 nchini Tanzania Bara na walimu 326 kutoka Zanzibar wamepatiwa mafunzo hayo.

UCSAF pia inashirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuboresha usikivu wa matangazo kwa kujenga vituo 19 vipya vya kurushia matangazo kwa kutumia ruzuku ya TZS bilioni 6.27.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mwasalyanda alibainisha kuwa serikali imeboresha ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kwa kununua vifaa vya kisasa vyenye thamani ya TZS milioni 200 ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa habari.
Pia UCSAF imetoa msaada wa vifaa vya TEHAMA kwa Shirika la Posta Tanzania, ili liweze kutoa huduma zake kidigitali. Mwezi Aprili 2025, UCSAF itakabidhi vifaa vingine 250 kwa Shirika hilo, mradi ambao una thamani ya TZS 161.9 milioni. Awali, tarehe 12 Julai 2024, UCSAF ilinunua na kukabidhi mashine 250 za PDA kwa shirika hilo.

Kwa upande wa upanuzi wa huduma za mawasiliano vijijini, UCSAF imeingia mikataba na watoa huduma kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi milioni 8.5 katika wilaya 127 zilizopo kwenye mikoa 26. Mradi huo umehusisha ujenzi wa minara 758 na kunufaisha kata 713 kwa kutumia ruzuku ya TZS bilioni 126.

Mhandisi Mwasalyanda alihitimisha kwa kusisitiza kuwa mafanikio haya ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza TEHAMA na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za mawasiliano.