Breaking News

TLP YAMPITISHA YUSUPH WANGIRA KUWA MGOMBEA URAIS UCHAGUZI MKUU 2025

Dar es Salaam — Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kimemchagua Yusuph Wangira kuwa mgombea wake wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Uchaguzi huo wa ndani ya chama umefanyika katika Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, Mwenyekiti wa uchaguzi, Coaster Jimmy, alisema jumla ya wapiga kura walikuwa 102 huku wagombea waliowania nafasi hiyo wakiwa watatu. Neema Nyerere alipata kura 6, Wilson Ella’s alipata kura 46, huku Yusuph Wangira akiongoza kwa kura 50 na hivyo kutangazwa rasmi kuwa mgombea urais kupitia chama hicho.
Akitoa shukrani kwa wanachama waliomchagua, Wangira aliwaahidi ushindi mkubwa kwa chama hicho kwenye nafasi ya urais, ubunge, na udiwani nchi nzima. Pia alimtambulisha mgombea mwenza wake, Amana Selemani Mzee, na kueleza kuwa watafanya kampeni za kistaarabu zenye lengo la kuleta mabadiliko chanya kwa taifa.
Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, aliwapongeza TLP kwa kuendesha uchaguzi huo kwa amani na kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia. Alisisitiza umuhimu wa wanachama kukubali matokeo na kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya chama. Aliongeza kuwa jumla ya vyama 18 vinatarajiwa kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na akatoa wito wa kudumisha amani na mshikamano miongoni mwao.

Hata hivyo, mmoja wa wagombea wa urais wa TLP, ambaye hakufanikiwa, alieleza kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi huo. Alidai kuwa idadi ya wapiga kura ilikuwa 170 na kwamba kati yao 13 walikuwa "mamluki", ambao alihusisha na kushindwa kwake.

TLP sasa inaingia katika hatua ya maandalizi ya kampeni za kitaifa huku macho ya Watanzania yakielekezwa kwenye mwelekeo wa kisiasa kuelekea Oktoba 2025.