Breaking News

WASOMI, WADAU KUJADILI UBIA WA SEKTA YA UMMA NA BINAFSI KATIKA DIRA YA TAIFA 2025

Na Mwandishi Wetu  - Wasomi na wadau mbalimbali watakutana kesho katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenye kongamano la kujadili nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila ambapo ameweka wazi kuwa mjadala huo utahusisha Wanazuoni kutoka UDSM watapata nafasi ya kutoa mchango wao kisomi.

Alisema PPPC kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti na Elimu kwa Demokrasia Tanzania (REDET) kitafanya kongamano hilo la siku moja Mei 27, 2025 katika jengo la Ukumbi wa Maktaba Mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi una nafasi kubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa uwezo wake wa kusaidia kujenga ustahimilivu dhidi ya misukosuko ya nje na changamoto za kifedha za umma” alisema Kafulila.

Kafulila alisema Serikali imeweka dhamira thabiti na yenye maono makubwa ya kuleta maendeleo makubwa nchini katika miaka ijayo kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hivyo ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPs) ni sehemu muhimu ya mpango wa maendeleo ya taifa.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Sekta Binafsi kama mhimili mkuu wa ukuaji wa uchumi imetiliwa mkazo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aidha, amesisitiza kuhusu umuhimu wa Tanzania kujitegemea kiuchumi kwa kupanua vyanzo vya kifedha kulingana na mabadiliko ya kimataifa katika njia za ufadhili wa maendeleo.

Alisema kongamano hilo linatarajiwa kujikita zaidi kwenye masuala kadhaa, ikiwemo masoko ya mitaji ya kimataifa, uhamasishaji wa kifedha, fursa pamoja na changamoto.

Kafulila alisema kongamano hilo litahusisha Watendaji Wakuu wa mashirika (CEOs), viongozi wa kibiashara pamoja na wadau wengine wa Sekta Binafsi pia wanatarajiwa kuhudhuria katika kongamano hili.

Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha nchini, hadi mwezi uliopita, Tanzania ilikuwa na miradi 80 ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPs) ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Serikali ya Tanzania tayari imeshatekeleza mageuzi mbalimbali ya kisheria na ya kikanuni yenye lengo la kurahisisha na kuhamasisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika Ubia na Sekta ya Umma.