WADAU WA USALAMA WATAKA MJADALA WA KITAIFA KIDHIBITI AJALI BARABARANI
Dar es salaam - Wadau wa usalama wa barabarani wametoa wito wa kuanzishwa kwa mjadala wa kitaifa kuhusu namna ya kudhibiti ajali za barabarani, wakisisitiza kuwa vifo na majeruhi vinavyotokana na ajali hizo, hususan kwa watoto, haviwezi kuvumilika tena katika jamii ya Watanzania.
Mwito huo umeungwa mkono leo, Mei 29, 2025, jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Miundombinu, Rogatus Mativila, wakati wa uzinduzi wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya usalama barabarani katika Shule ya Msingi Sinza Maalum, mradi unaotekelezwa na Shirika la Amend Tanzania.
Mativila amesema ajali za barabarani zimeendelea kuleta huzuni kwa jamii, hasa pale watoto wanapopoteza maisha au kujeruhiwa katika mazingira ya shule, na hivyo ni wakati muafaka kwa taifa kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu namna ya kukabiliana na tatizo hilo.
Amesema serikali kupitia TAMISEMI itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha shule zinakuwa maeneo salama kwa watoto, ikiwa ni pamoja na kuweka vivuko vya watembea kwa miguu, matuta ya kupunguza mwendo, na alama za barabarani katika maeneo ya shule.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Amend Tanzania, Simon Kalolo, amesema mradi huo ni wa kipekee kwani kwa mara ya kwanza unatekelezwa kwenye shule yenye wanafunzi wenye mahitaji maalum pekee. Ameeleza kuwa ajali za barabarani husababisha vifo vya takriban watu milioni 1.3 duniani kila mwaka, huku zaidi ya milioni 50 wakijeruhiwa
na kuwa chanzo kikuu cha vifo kwa watoto na vijana wenye umri wa miaka 5 hadi 29.
Kalolo amesema mpaka sasa, mradi wa Amend umefikia shule 59 nchini Tanzania kati ya shule 100 barani Afrika, na kunufaisha wanafunzi zaidi ya 52,793 nchini Tanzania na zaidi ya 102,000 barani Afrika.
Naye Mwakilishi wa Jeshi la Polisi kutoka Kitengo cha Usalama Barabarani, SSP Mbunja Matibu, amesema jeshi hilo linaendelea kutoa elimu ya usalama kwa watoto na watu wazima mashuleni, sambamba na kuhimiza jamii kuwajibika katika kuhakikisha usalama wa watoto barabarani.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam anayeshughulikia Elimu, Abedi Milanzi, amesema maboresho ya miundombinu hiyo yamepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za usalama kwa watoto wenye mahitaji maalum katika shule hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya FIA Foundation, Saul Billingsley, amepongeza juhudi za Amend Tanzania na kusema kuwa amevutiwa na dhamira ya shirika hilo ya kuwalinda watoto dhidi ya ajali.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, amesema tatizo la ajali limekuwa kubwa wilayani humo, akitolea mfano Hospitali ya Mwanyamala kuwa inapokea wastani wa watu wawili waliopoteza maisha kila siku kutokana na ajali, sawa na vifo 60 kwa mwezi.
Miundombinu iliyowekwa katika Shule ya Msingi Sinza Maalum ni pamoja na matuta ya kupunguza mwendo kasi, vivuko vya watembea kwa miguu, alama za barabarani, na njia maalum za watembea kwa miguu, ikiwa ni hatua ya kulinda usalama wa wanafunzi, hususan wenye mahitaji maalum








