WAZIRI KOMBO AWASISITIZA MACHIFU KUSHIRIKIANA NA SERIKALI
Dodoma - Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasisitiza Machifu wa Kanda ya Vita ya Majimaji Kusini mwa Tanzania kuendelea kushirikiana na Serikali wakati wakitekeleza majukumu yao ya kimila katika jamii.
Hayo yamejiri wakati Waziri Kombo alipokutana na ujumbe huo wa machifu katika ofisi za Wizara jijini Dodoma na kuzungumza nao masuala mbalimbali ya kimkakati ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hususan Diplomasia ya Utamaduni.
Wakieleza lengo la ujio wao, Machifu hao wameeleza kiu ya kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kuhakikisha nchi inakuwa na utulivu na amani hususan katika maeneo ya mipakani kupitia ushirikiano walionao na machifu wa nchi jirani ili kuenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru ya kueleta amani nje ya mipaka na kuisisitiza jamii kuifanyia kazi falsafa hiyo muhimu.
Pia, wameeleza maeneo yenye tija katika ushirikiano wa machifu hao na machifu wa nchi jirani ni pamoja na kupeana taarifa za tahadhari na fursa mbalimbali zenye manufaa kwa wananchi wao ikiwemo; taarifa za biashara haramu, kusaidia operesheni za amani na ulinzi, utunzaji wa mazingira, tahadhali za ukame na ukosefu wa chakula na kukuza matumizi ya lugha ya kiswahili.
Chief Hangaya Mtembele Festival linalotarajiwa kufanyika mkoani Mtwara ambalo litatumika kutangaza fursa mbalimbali za utalii na historia ya utamaduni katika ukanda huo wa kusini. Tamasha hilo litashirikisha kabila la wayao kutoka katika nchi za kusini mwa Afrika za Msumbiji, Zambia, Zimbabwe na Malawi.
Naye Waziri Kombo amewahakikishia machifu hao kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nao katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje na kwamba watambue kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameupa umuhimu mkubwa umoja wa machifu nchini na kila mwaka amekuwa akishiriki tamasha la machifu ili kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma za machifu nchini








