PIN NA TMC WAPENDEKEZA KULINDWA HAKI ZA KIDIJITALI KUELEKEA UCHAGUZI 2025
Dar es salaam - Mashirika Yatakiwa TCRA Kurejesha Upatikanaji wa Mtandao wa X na Kuheshimu Haki za Kidijitali kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Mashirika mawili yanayoongoza katika kutetea haki za kidijitali, Paradigm Initiative (PIN) na Tech & Media Convergency (TMC), yametoa mapendekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kurejesha kikamilifu upatikanaji wa mtandao wa X (zamani Twitter), pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa intaneti iliyo wazi, jumuishi, na isiyozuiliwa kabla, wakati, na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.
Mapendekezo hayo yametolewa leo Mei 29, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa TMC, Asha Abinallah, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliotanguliwa na warsha ya siku mbili ya Digital Rights and Elections in Africa Monitor (DREAM) – Toleo la Tanzania. Warsha hiyo ililenga kuangazia changamoto na vikwazo vinavyoendelea kuathiri haki za kidijitali katika muktadha wa uchaguzi.
Bi. Abinallah alieleza wasiwasi wa mashirika hayo kuhusu hali ya haki za kidijitali na nafasi ya kiraia, hasa katika maeneo ya uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa taarifa, na uhuru wa vyombo vya habari mtandaoni. Alitoa wito kwa TCRA kuhakikisha kuwa majukwaa ya kidijitali hayaondolewi au kuzimwa kiholela, na kuhimiza ulinzi wa uhuru wa kujieleza kama inavyolindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, alipendekeza matumizi ya lugha za kienyeji katika utoaji wa taarifa za uchaguzi ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kufahamu taarifa hizo kwa urahisi. Kwa upande wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), aliitaka Tume hiyo kufuatilia na kuripoti kwa uwazi ukiukwaji wa haki za kidijitali katika kipindi chote cha uchaguzi, pamoja na kushirikiana na asasi za kiraia katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi salama na ya haki ya mitandao.
Kwa upande mwingine, kampuni za mawasiliano zimetakiwa kuhakikisha utulivu wa huduma za mitandao wakati wa uchaguzi na kutoa taarifa kwa umma kuhusu maagizo yoyote ya serikali yanayohusu kuzimwa kwa mitandao au kudhibiti maudhui. Bi. Abinallah alisisitiza umuhimu wa uwazi kwa kuchapisha ripoti za mara kwa mara kuhusu maombi ya serikali yanayohusiana na taarifa au maudhui ya mtandaoni.
"Tuna dhamira ya kuona Tanzania inaingia kwenye kipindi hiki muhimu cha kidemokrasia ikiwa na mazingira ya kidijitali ambayo ni jumuishi, shirikishi, na yenye kuheshimu haki," alisema Abinallah.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Paradigm Initiative, Bw. Gbenga Sesan, alieleza kuwa Mpango wa DREAM ni sehemu ya mradi wa bara zima unaolenga kufuatilia, kuhifadhi kumbukumbu, na kutoa majibu dhidi ya ukiukwaji wa haki za kidijitali nyakati za uchaguzi. Aliongeza kuwa toleo la Tanzania linaendeleza juhudi zilizofanyika wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024, na linakwenda sambamba na Mkutano wa 2025 wa Utawala wa Mtandao Afrika (AfIGF).




