Breaking News

MADELEKA AJITOSA RASMI KUGOMBEA UBUNGE KIVULE KUPITIA ACT WAZALENDO

Dar es Salaam, Mei 31 — Mwanasiasa na mwanaharakati maarufu, Peter Madeleka, ametangaza rasmi kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kivule kupitia Chama cha ACT Wazalendo. Alichukua fomu ya kugombea leo mbele ya wanachama na viongozi wa chama hicho, katika hafla iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa wafuasi na wakazi wa jimbo hilo.

Akihutubia mkutano huo, Madeleka aliahidi kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi wa Kivule, akieleza kuwa hali ya maisha kwa sasa ni ngumu kutokana na kile alichokiita "kutokuwepo kwa uongozi bora wa Chama cha Mapinduzi (CCM)."

> "Wananchi wamechoka na hali ngumu ya maisha. Miundombinu ni mibovu, bei za bidhaa zipo juu, huduma za afya na elimu ni duni. Haya yote ni matokeo ya mfumo wa uongozi wa CCM," alisema Madeleka.
Amehimiza wananchi kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kidemokrasia badala ya kulalamika pembeni, akisema huu ni wakati wa kupigania mabadiliko.

"Hatuwezi kususa tunapaswa kushiriki, kupigania, na kushinda mabadiliko," alisisitiza.
Madeleka aliwasili katika hafla hiyo akisindikizwa na viongozi wa ACT Wazalendo wa ngazi ya wilaya na mkoa, pamoja na wafuasi wake waliokuwa wakipaza kauli mbiu za mabadiliko na matumaini mapya kwa Jimbo la Kivule.

Hatua ya Madeleka kuingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha ubunge inatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa katika jimbo hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.