KITUO CHA UHUSIANO WA KIMATAIFA CHA DKT. SALIM AHMED SALIM KINARA UTOAJI WA MAFUNZO YA DIPLOMASIA NA LUGHA
Dodoma, Mei 28, 2025 – Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amewaeleza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kimedumu kuwa kinara katika utoaji wa mafunzo ya diplomasia na lugha nchini.
Akisikiliza Hotuba ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2025/2026, Balozi Kombo alibainisha mafanikio ya kituo hicho katika mwaka wa masomo 2024/2025:
Jumla ya wanafunzi waliojiandikisha: 1,646
Astashahada ya awali: 149
Astashahada: 131
Stashahada: 120
Stashahada ya juu: 840
Shahada: 251
Stashahada ya uzamili: 155
Aidha, Kituo kinaendesha kozi za lugha za kigeni saba (7), zikiwemo Kiarabu, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza, Kichina, Kikorea na Kireno. Mbali na hayo, kipo na mafunzo ya muda mfupi katika maeneo ya diplomasia, uhusiano wa kimataifa, stratejia, usuluhishi wa migogoro na ujenzi wa amani.
Balozi Kombo pia alifahamisha Bunge kuwa katika mwaka uliopita, Kituo kilifanikiwa kuwahudumia washiriki 221 kutoka sekta za umma na binafsi kupitia mafunzo ya muda mfupi, hatua ambayo inalenga kuinua uwezo wa wataalamu wa mahusiano ya kimataifa na diplomasia nchini.
“Serikali itaendelea kuimarisha na kupanua kituo hiki ili kukidhi mahitaji yanayokua ya mafunzo ya kitaaluma na kitaalamu katika nyanja za diplomasia na lugha,” alisema Mhe. Kombo.
Kwa mujibu wa Wizara, mkakati wa kuongeza rasilimali, kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali wa kimataifa na kuboresha miundombinu utaendelea kuimarisha mamlaka ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kama kitovu cha mafunzo ya kitaaluma nchini.




