CUF : ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA KWA VYAMA VYA SIASA NI KINYUME CHA KATIBA NA HALIKUBALIKI
Na Mwandishi Wetu - Chama Cha Wananchi CUF, kimeeleza kupinga kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusu kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, kikisema hatua hiyo ni kinyume cha Katiba na sheria, huku ikionya kuwa inaweza kuchochea mvutano wa kisiasa nchini.
Katika taarifa iliyotolewa Juni 26, 2026 na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Eng. Mohamed Ngulangwa, CUF imesema imepokea kauli hiyo kwa mshangao na masikitiko, ikieleza kuwa haikubaliki katika kipindi ambacho taifa bado linaendelea kukabiliana na athari za matukio ya vurugu ya Oktoba 29, 2025.
Chama hicho kimekumbusha kuwa mwaka 2024 Rais Samia Suluhu Hassan aliweka wazi kuwa mikutano ya hadhara ni haki ya kikatiba na kisheria kwa vyama vya siasa, hivyo kuizuia si sahihi. Kwa msingi huo, CUF imesema kauli ya Waziri Patrobas Katambi haiwezi kuwa juu ya msimamo wa Rais wala Katiba ya nchi.
Aidha, CUF imesema iliwahi kuishauri Serikali ya Awamu ya Tano kutokandamiza demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria, ikionya kuwa kufanya hivyo kungehatarisha utulivu wa nchi. Chama hicho kinasema bado taifa linaendelea kubeba athari za mgogoro uliotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Pia, CUF imekumbusha kuwa miezi miwili iliyopita Mwenyekiti wa chama hicho, Mirambo Camil Yusuf, alipongeza mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande kuhusu Uponyaji na Maridhiano. Kwa mujibu wa chama hicho, utekelezaji wa mapendekezo hayo unapaswa kuanza kwa kuheshimu haki za msingi za kisiasa badala ya kuendelea kuzibana.
CUF imesisitiza kuwa jukumu la Jeshi la Polisi katika mikutano ya hadhara si kutoa kibali bali kupokea taarifa za mikutano na kuhakikisha ulinzi na usalama vinadumishwa wakati wa mikutano hiyo.
Chama hicho pia kimetoa wito kwa Serikali kusikiliza madai ya wananchi badala ya kuyapuuza, huku kikitaka mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande kuhusu kuharakishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya ya wananchi yaanze kutekelezwa. Kimeeleza kuwa Katiba Mpya yenye misingi imara ya demokrasia na utawala bora ndiyo suluhisho la kudumu la changamoto za kisiasa nchini.
Mwisho, CUF imesisitiza kuwa Tanzania inahitaji maridhiano ya kweli yanayojengwa juu ya haki, demokrasia na utawala bora, badala ya hatua zinazoweza kuongeza mvutano wa kisiasa.




