Breaking News

ADC KUFANYA MKUTANO MKUU MAALUMU WA UTEUZI WA WAGOMBEA JUNE 29

Dar es salaam - Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu Maalum tarehe 29 Juni 2025 kwa ajili ya kuwateua wagombea watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa ADC, Mwalimu Hamad Azizi, amesema mkutano huo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya chama hicho katika kuhakikisha kinawapisha wagombea imara na wenye uwezo wa kushindana kwa nafasi mbalimbali.

"Tutapitisha wagombea kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa nafasi zote za uongozi, ili kuhakikisha tunashiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi na kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi," amesema Mwalimu Azizi.

Ameeleza kuwa hadi kufikia Juni 26, 2025, jumla ya wagombea watatu wamechukua fomu za kugombea nafasi ya Urais kupitia chama hicho. Kwa upande wa Tanzania Bara, waliotia nia ni Muttamwega Mgaywa na Wilson Mulumbe, huku kwa upande wa Zanzibar fomu imechukuliwa na Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, Ahmad Rashid.

Mwalimu Azizi amesisitiza kuwa mchakato wa uteuzi wa wagombea hao utaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya uwazi, demokrasia ya kweli, na haki, ili kila mgombea apate nafasi sawa ya kushindanishwa kwa usawa na uadilifu.

Chama cha ADC kimedhamiria kutoa mfano bora wa uendeshaji wa siasa za kistaarabu na kuchochea mabadiliko ya kweli kwa manufaa ya wananchi.