Breaking News

SHEIKH JALALA ATOA SALAMU ZA MWAKA MPYA WA KIISLAMU 1447–2025

# Watanzania Waaswa Kuienzi Amani, Umoja na Mshikamano Huku Uchaguzi Mkuu Ukikaribia

Dar es Salaam – Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna’ashariyyah Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala, ametoa salamu za heri na baraka kwa Waislamu wote nchini katika kuadhimisha mwaka mpya wa Kiislamu 1447 Hijria, unaoanza rasmi mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari, Sheikh Jalala amewataka Watanzania wote, hususan Waislamu, kuendelea kuienzi tunu ya amani, umoja na mshikamano, hasa tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

"Kama Waislamu, tunayo kalenda yetu tukufu. Mwaka mpya wa Kiislamu si tu tukio la kihistoria bali ni fursa ya kujitathmini na kujitahidi kuwa bora zaidi katika uchaMungu, mshikamano na maadili ya kijamii," alisema Sheikh Jalala.

Sheikh Jalala alitaja mambo matano muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika maadhimisho ya mwaka huu mpya, akianzia na kuimarisha kwa nguvu umoja na ushirikiano baina ya madhehebu yote ya Kiislamu nchini.

“Mwaka huu 1447 ukawe ni mwaka wa kudumisha umoja na ushirikiano kati ya madhehebu yote ya Kiislamu, na Watanzania kwa ujumla, kwa kuhakikisha kuwa tunalinda na kuimarisha mshikamano wetu wa kitaifa,” alisema Sheikh Jalala.

Aidha, alisisitiza kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madhehebu mbalimbali ya dini kama vile Shia, Sunni na wengineo, na kwamba tofauti hizo ni neema na hazipaswi kuwa chanzo cha migawanyiko bali msingi wa kujenga taifa lenye heshima, haki na maendeleo ya pamoja.

Mwisho, Sheikh Jalala aliwatakia Waislamu wote nchini na duniani kwa ujumla mwaka mpya wenye kheri, baraka, mafanikio na utulivu wa kijamii na kisiasa.