BAKARI KIMWANGA ACHUKUA NA KURUDISHA FOMU YA UDIWANI KATA YA MAKURUMLA
Dar es Salaam — Mwanahabari na Diwani wa Kata ya Makurumla anayemaliza muda wake, Bakari Kimwanga, ameonesha nia ya kuendelea kulitumikia eneo hilo kwa muhula mwingine baada ya kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kimwanga alikabidhi fomu hiyo kwa Katibu wa CCM wa Kata ya Makurumla, Omari Suleiman Bakari, ambapo aliwataka wananchi na wanachama wa CCM kuendelea kumuunga mkono ili kukamilisha miradi iliyobakia.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo, Kimwanga alisema anajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake cha uongozi, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 18.
“Ninamaliza miaka mitano ya mafanikio ambapo sisi Makurumla tumetekeleza miradi mikubwa ya barabara, kituo cha afya na elimu,” alisema Kimwanga.
Aliongeza kuwa endapo atapata ridhaa ya chama na wananchi, ataendelea kusukuma maendeleo kwa kasi zaidi katika kipindi kijacho.
“Miaka mitano ijayo tunakwenda kujenga kata yenye kasi zaidi na muonekano mkubwa wa maendeleo kwa jamii. Wana Makurumla na wana CCM ni watu wema sana, nyakati zote tumekuwa pamoja. Mungu akipenda na chama kikiridhia jina likarudi kwenye uteuzi, sina shaka – kwa chama chetu ni ushindi,” alisisitiza Kimwanga.
Kimwanga anajiunga na idadi ya wagombea wanaowania nafasi mbalimbali katika mchakato wa ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.








